Rais Samia aomboleza kifo cha Nyamo-Hanga, dereva wake

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ameomboleza kifo cha Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Gissima Nyamo-hanga pamoja na dereva wake, Muhajiri Haule kilichotokea usiku wa kuamkia leo wilayani Bunda mkoani Mara.

Rais Samia kupitia mitandao yake ya kijamii leo Aprili 13, 2025 ameandika: “Nimepokea kwa masikitiko taarifa ya vifo vya Mhandisi Boniface Gissima Nyamohanga, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), pamoja na dereva wake, Muhajiri Mohammed Haule, vilivyotokea usiku wa kuamkia leo kwa ajali ya barabarani eneo la Bunda, Mkoa wa Mara.

“Ninatoa pole kwa familia, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko, watumishi wa Tanesco, ndugu jamaa na marafiki.”

Pia ameongeza: “Namuomba Mwenyezi Mungu azijaalie familia, ndugu, jamaa na marafiki subira, uvumilivu na moyo wa ibada katika kipindi hiki kigumu. Mwenyezi Mungu azilaze roho zao mahali pema peponi.”

Nyamo-hanga aliteuliwa na Rais Samia kushika wadhifa huo Septemba 23, 2023 akichukua nafasi ya Maharage Chande, kabla ya uteuzi huo alikuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Umeme Vijijini (Rea).

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *