Dar es Salaam. Baada ya kutoka kuiondoa Al Masry katika hatua ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, Simba itakuwa na kibarua kingine dhidi ya Mbeya City leo saa 10:00 jioni katika mechi ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB kwenye uwanja wa KMC Complex, Mwenge, Dar es Salaam.

Simba ilifuzu kwenda katika hatua ya robo fainali baada ya kuifunga Bigman mabao 2-1 wakati Mbeya City ilifuzu baada ya kupata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Mtibwa Sugar.
Mchezo wa leo hautazamiwi kuwa mwepesi kwani Mbeya City imekuwa na mwendelezo mzuri msimu huu katika Ligi ya Championship ambapo inashika nafasi ya pili ikiwa na pointi 56 nyuma ya Mtibwa Sugar ambao ndiyo vinara wakiwa na pointi 63.

Mara ya mwisho Simba kukutana na Mbeya City ilikuwa 2023 kwenye Ligi Kuu ambapo Wekundu wa Msimbazi waliibuka na ushindi wa mabao 3-2.
Simba imekutana na Mbeya City katika michezo 20 yote ikiwa ya Ligi Kuu ambapo Mbeya City imeshinda mechi tatu na kupata sare mechi nne na Simba imeshinda mechi 13.
Kocha msaidizi wa Simba, Selemani Matola amesema wamejiandaa kuikabili Mbeya City na wataingia uwanjani kucheza kwa tahadhari.
“Tunaenda kucheza kama fainali na kuhakikisha tunaingia nusu fainali. Njia waliyopita Mbeya City mpaka kufika hapa hawakubahatisha kwani waliitoa Azam na mpaka wamefika hapa ni tuimu ambayo ni ngumu kwa hiyo tumejipanga pamoja na ugumu wao tunahitaji kupata matokeo,” amesema Matola.