
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ambacho ndicho chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania, hakijasaini kanuni za maadili ya uchaguzi mkuu 2025, ikiashiria hakipo tayari kushiriki uchaguzi chini ya sheria za sasa za uchaguzi.
Chadema hakitakuwa chama cha kwanza cha upinzani kususia uchaguzi kwani mwaka 2017 wakati wa marudio ya uchaguzi, nafasi ya Rais huko Kenya, mwanasiasa mkongwe katika siasa za Kenya, Raila Odinga alisusia uchaguzi huo.
Nikimnukuu alisema: “We cannot legitimize a sham election. We are not part of it”, akimaanisha kuwa “Hatuwezi kuhalalisha uchaguzi bandia. Sisi si sehemu yake,” alisema Odinga.
Lakini pamoja na msimamo wa Chadema wa kutokuwepo uchaguzi endapo mabadiliko ya sheria za uchaguzi hayatafanyika, wapo baadhi ya viongozi waliopitisha vuguvugu hilo, wanaona bora waingie katika uchaguzi na sheria hizo hizo mbaya.
Morgan Tsvangirai wa Zimbabwe naye mwaka 2008 aliwahi kususia uchaguzi na akatamka maneno yafuatayo: “Conditions for a free and fair election do not exist. Participating would be to endorse the violence”, mwisho wa kunukuu.
Kwa tafsiri isiyo rasmi, Tsvangirai alisema “Mazingira ya uchaguzi huru na wa haki hayapo. Kushiriki itakuwa ni kuidhinisha vurugu,” na kutokana na kauli hiyo alijitoa katika uchaguzi mkuu na kumwacha Rais Robert Mugabe. Sasa wote ni marehemu.
Hao sio wanasiasa pekee waliowahi kususia uchaguzi kwani mwaka 2010, mgombea wa urais wa Myanmar, Aung San Suu Kyi alipata kusema: “If the elections is sham, and partcipation would mean giving them legitimacy”.
Kwa tafsiri isiyo rasmi, kama uchaguzi ni bandia, kushiriki ni kuwapa uhalali.
Katibu mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa (UN), aliwahi kusema “Elections are not just about voting. They are about trust. They are about the process”, akimaanisha uchaguzi sio tu kitendo cha kupiga kura, bali ni ule mchakato.
Kuna usemi “kuvuja kwa pakacha nafuu ya mchukuzi” ikimaanisha pengine chama tawala (CCM) kikapata ushindi wa mteremko na vyama visivyo na umaarufu vikapata viti vya ubunge na udiwani, hii huwa ni hulka ya mwanadamu.
Kwa wanaofahamu kidogo somo la sayansi ya siasa, pale chama kikuu cha upinzani kinaposusia uchaguzi kutokana na madai ya ukiukwaji wa haki, huwa ina madhara makubwa kisiasa, kijamii na kimataifa kama ambavyo nitaeleza baadaye.
Duniani, wataalamu wa sayansi ya siasa wanaainisha ukiukwaji wa haki katika uchaguzi kuwa ni pamoja na mfumo wa uchaguzi unaochezewa kirahisi, upendeleo wa Tume ya Uchaguzi na mifumo mibaya ya sheria za uchaguzi.
Hebu tujiulize nini ambacho kimeifanya Chadema kudai mabadiliko ili kiweze kushiriki uchaguzi, hasa tukitumia mifano ya chaguzi za Serikali za Mitaa 2019 na 2024 na uchaguzi mkuu 2020, ili tutafakari kama madai yao yana msingi au la.
Tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa hapa Tanzania mwaka 1992, vyama vya upinzani kikiwamo Chadema, vimekuwa vikililia kubadilishwa kwa mfumo wa uchaguzi, vikidai mfumo uliopo sasa unapendelea upande mmoja.
Si vyama vya upinzani tu, lakini hata viongozi wa dini, wanaharakati na baadhi ya wananchi walitamani Katiba ya Tanzania iandikwe upya ili pamoja na mambo mengine, iwezeshe kupatikana kwa Tume Huru ya Uchaguzi kwa sifa, sio jina.
Walitaka pia kuruhusiwa kwa mgombea binafsi, matokeo ya Rais kuhojiwa mahakamani, Rais ashinde kwa asilimia 50+ na mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi, makamu wake na watendaji kuomba kazi kwa sifa na si kuteuliwa.
Tume Huru ambayo haitaruhusu watumishi wa umma, hasa wakurugenzi wa halmashauri ambao baadhi ni makada, kusimamia chaguzi kutokana na wasimamizi hao kuhakikisha wanalinda masilahi ya Chama cha Mapinduzi.
Lakini siku nne zilizopita, makamu Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu ambaye sasa yuko mahabusu kwa tuhuma za uhaini zilizoanzia katika vuguvugu la kisiasa la kudai mabadiliko ya mifumo ya uchaguzi, alionekana kama kulegeza masharti.
Lissu akatangaza mambo sita kama yatarekebishwa walikuwa wapo tayari kushiriki uchaguzi huu mkuu wa 2025 ambayo ni pamoja na kusiwe na mgombea anayepita bila kupingwa na kuzuia taratibu zinazoruhusu baadhi ya wagombea kuenguliwa.
Lakini alienda mbali na kusema hawataki watoto wadogo kuandikishwa kwenye daftari la kudumu la mpigakura, hawataki kufanyiwa fujo kwenye kampeni, mawakala wafanye kazi zao kwa uhuru na kusiwepo mauaji ya kisiasa.
Kwa mtu yeyote mwenye akili na mpenda demokrasia wa kweli atakubaliana na mimi kuwa Lissu, Chadema na vyama vichache makini vya upinzani, wanayo hoja ya msingi, lakini wenye mamlaka ni kama wameamua kuziba masikio.
Sasa Chadema wamefikishwa mahali wanaona hakuna haja ya kuingia katika uchaguzi ambao sanduku la kura haliamui mshindi, bali anayehesabu na kutangaza matokeo, bado vipo vyama vitachelekea bila kufahamu madhara yake.
Sote tunakubaliana kuwa kwa takwimu, Chadema kwa sasa ndicho chama kikuu cha upinzani kwa sababu hata takwimu zinakibeba kuhusu kukubalika kwake.
Katika uchaguzi mkuu 2005, mgombea urais wa Chadema, Freeman Mbowe alipata kura asilimia 5.88, mwaka 2010, mgombea wao Dk Willibrod Slaa akapata asilimia 26.34 na mwaka 2015, Edward Lowassa akapata asilimia 31.5.
Sitauzungumzia uchaguzi wa 2020 kutokana na mazonge yake, lakini kwa takwimu hizo, Chadema ndicho kimekuwa kikishika namba mbili tangu uchaguzi mkuu 2010 hadi uchaguzi mkuu wa 2020 ambao kila Mtanzania anajua nini kilitokea.
Sasa kama kweli Chadema watasusia uchaguzi huu kwa mujibu wa wataalamu wa sayansi ya siasa, kunaweza kujitokeza mgogoro wa uhalali wa kisiasa na ndani na kimataifa wanaweza kuchukulia aliyeshinda kama hana uhalali wa kisiasa.
Mtu anaweza kujitokeza na kusema utakosaje uhalali wa kisiasa wakati kuna vyama vingine 17 vya upinzani vimeshiriki, lakini mwenye mawazo hayo tutamuuliza, vyama hivyo viliwahi kushinda nini kulinganisha na Chadema.
Lakini athari nyingine ya kisiasa ni kuwa hata kama chama tawala kama ilivyo CCM hapa nchini kitashinda, ile kukosekana kwa ushindani (kama tunaoushuhudia kati ya CCM na Chadema), kunaweza kuleta matokeo ya kutopata uhalali kisiasa.
Mbali na hilo, wataalamu wa sayansi ya siasa na hii si kwa Tanzania pekee bali ni duniani, wanasema kutoshiriki kwa chama kikuu cha upinzani kunaweza kuimarisha udikteta, kama mgomo hautasaidia kuleta shinikizo kimataifa.
Lakini inaweza kusababisha umma upoteze imani na mfumo mzima wa uchaguzi na kusababisha idadi ya wanaojitokeza kupiga kura kupungua na mgomo huo unaweza kusababisha nchi ikawekewa vikwazo kuishinikiza kurudi kwenye haki.
Ukiacha hivyo kama nilivyotangulia kusema nilipotumia usemi wa kuvuja kwa pakacha nafuu ya mchukuzi, mgomo wa chama kikuu cha upinzani unaweza kusababisha mgawanyiko wa vyama vya upinzani na vingine kuona ni fursa.
Lakini kususia uchaguzi kunaweza kukifanya chama kikuu cha upinzani kukosa viti vya udiwani na ubunge na kukifanya kipoteze ule ushawishi wa kuikosoa serikali na pia hata kukosa ruzuku ambayo ingekipa nguvu kutekeleza mipango yake.
Katika nchi nyingine duniani, mgomo wa chama kikuu cha upinzani unaweza ukafuatiwa na migomo ya umma, raia kutotii Serikali na hata wakati mwingine nchi kutumbukia kwenye machafuko na umwagaji wa damu.
Kwa hali tuliyonayo sasa, badala ya kufurahia Chadema kuwekwa kando, tungetafakari kama taifa iwapo kile wanachokidai ni halali au si halali, ili sasa kama taifa tutafute maridhiano kabla kuingia kwenye uchaguzi.
Tusikichukulie poa Chadema kwamba kwa kususia kanuni kinaenda kufa wakati hakuna anayefahamu mipango yao ya baadaye kwa sababu waswahili wanasema ukiona kobe ameinama ujue anatunga sheria, sisi yetu ni macho.
0656600900