Diaspora watakiwa kuwekeza nchini

Dar es Salaam. Watanzania waishio nje ya nchi (Diaspora), wametakiwa kutosita kuwekeza na kutuma fedha nchini kwa kuwa, wadau wa huduma za kifedha kwa kushirikiana na Serikali wamewatengenezea njia rahisi ya kufanikisha hayo.

Hayo yamebainishwa mwishoni mwa wiki hii na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Cosato Chumi ambaye ametoa wito kwa Watanzania hao kuchangamkia fursa ya kuwekeza nyumbani, akisema mchango wao ni nguzo muhimu ya maendeleo ya Taifa.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Cosato Chumi.

Ametoa wito huo katika hafla ya uzinduzi wa Akaunti ya Mzawa ya Benki ya Absa Tanzania ambayo ni huduma kamili ya kibenki kwa Watanzania wanaofanya kazi na kusoma nje ya nchi.

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Chumi ameipongeza Absa kwa ubunifu wa huduma hiyo inayolenga kupunguza changamoto wanazokutana nazo Watanzania wanaoishi ughaibuni, hususan katika kupata huduma za kifedha, kutuma fedha na kushiriki katika uwekezaji wa ndani.

Kwa mujibu wa takwimu kutoka Idara ya Masuala ya Diaspora, zaidi ya Watanzania 400,000 wanaishi nje ya nchi, wengi wao wako Marekani, Uingereza, Kanada, Ulaya, Mashariki ya Kati, na kusini mwa Afrika.

Mwaka 2022 pekee, Watanzania waishio ughaibuni walituma Dola 598 milioni za Marekani kurudi nyumbani, (Sh1.4 trilioni), huku zaidi ya Sh6.4 bilioni zikitumika kununua mali.

Chumi amekiri mchango mkubwa wa diaspora pamoja na changamoto wanazokumbana nazo.

“Diaspora yetu haijajitenga imewekeza kwa dhati,lakini kwa bahati mbaya, hawapati fursa za kutosha kushiriki ipasavyo. Na sisi kama Serikali tunasema tumewasikia. tunawaona na tunachukua hatua.

“Chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, Serikali imepiga hatua kubwa kupitia huduma za ubalozi kwa njia ya kidijitali, majukwaa ya uwekezaji ughaibuni na sasa kuhimiza benki kama Absa kuunda huduma mahsusi kwa diaspora,”amesema Chumi.

Aidha, ameipongeza Absa kwa kutoa suluhisho la wakati, jumuishi na lenye tija akisema Akaunti ya Mzawa ya Absa inawaleta pamoja kila kitu ambacho diaspora imekuwa ikikiomba.

“Kwa Watanzania wote waishio nje ya nchi, nawaambia, muda ni huu. Miundombinu inajengwa. Msaada unazidi kuongezeka. Tuchukue hatua sasa tujenge nyumba, tufungue biashara, tuwekeze, na tujikite nyumbani Tanzania,”amesema Chumi.

Mkurugenzi Mtendaji wa Absa Tanzania, Obedi Laiser amesema Akaunti ya Mzawa imelenga kuondoa changamoto zilizodumu kwa muda mrefu zinazowakabili Watanzania, ikiwa ni pamoja na ugumu wa kupata huduma za kifedha, changamoto za kufungua akaunti za fedha za kigeni na upungufu wa taarifa za fursa na msaada wa mbali.

Huduma hii inatoa upatikanaji wa kimataifa wa akaunti kwa sarafu tano (TZS, USD, GBP, EUR na ZAR), kufanikisha miamala rahisi, fursa za uwekezaji na huduma za bima kupitia Absa Bima.

“Hii si tu bidhaa ya kifedha ni kiunganishi. Ni daraja la kifedha linalowaunganisha Watanzania wa ughaibuni na nyumbani,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *