Mnoga agonganisha mabosi England

MWEZI mmoja kabla ya mkataba wake na Salford City ya England kutamatika mwezi ujao (Mei), beki wa kimataifa wa Tanzania, Haji Mnoga ameanza kuwachonganisha viongozi wa timu hiyo.

Mnoga alijiunga na Salford City kwa mkataba wa mwaka mmoja wenye kipengele cha kuongezeka ikiwa mchezaji huyo ataonyesha kiwango bora.

Mwendelezo wa kiwango alichoonyesha beki huyo wa pembeni tangu mwanzoni mwa msimu umeanza kuwaumiza vichwa viongozi wa klabu hiyo ambayo inatamani kuendelea nae msimu ujao.

Uwezo alionao wa kukaba na kupeleka mashambulizi kwa wapinzani umemfanya aanze kugeuka kuwa lulu kwenye kikosi hicho kilichopo nafasi ya tisa kwenye msimamo wa ligi hiyo yenye timu 24.

Beki huyo amecheza mechi 34 za mashindano yote akifunga bao moja na kutoa asisti nne kwenye Ligi daraja la nne.

Mchezo wake wa kwanza alicheza kwa dakika 11 dhidi ya MK Dons Septemba 02 mwaka jana na tangu hapo amekuwa akipata nafasi ya kuanza kikosini hapo.

Kwa sasa ndiye beki tegemeo wa klabu hiyo akianza na kumaliza dakika zote 90 chama hilo likiruhusu mabao 47 kwenye mechi 41 ilizocheza.

Mwanaspoti ilizungumza na mmoja wa watu wa karibu wa mchezaji huyo (jina tunalo) akisema; “Salford imemuandalia ofa nono Mnoga kutokana na mwenendo wake huenda akasalia msimu ujao itategemea kama mwenyewe atakubali ofa hiyo.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *