
KOCHA Mkuu wa TMA FC, Mohamed Ismail ‘Laizer’, amesema mkakati uliopo kwa sasa ni kupata pointi 12, katika michezo minne iliyobaki kumalizia msimu huu, licha ya kukiri changamoto kubwa itakuwa ni kupambana na wapinzani wao wakicheza ugenini.
Katika michezo minne iliyobaki ya kumaliza msimu kwa kikosi hicho, itakuwa na miwili nyumbani ambayo ni dhidi ya Kiluvya United Aprili 20, kisha Bigman FC (Mei 10), huku ya ugenini ni mbele ya Transit Camp Aprili 26 na Mbeya Kwanza Mei Mosi.
“Mkakati wetu ni kupata pointi 12 katika michezo hiyo ingawa haitokuwa rahisi kutokana na ushindani na uhitaji wa kila timu, tunaweza kumaliza nafasi nne za juu, hivyo tutapambana ili tupate nafasi ya kucheza ‘Play-Off’,” alisema Mohamed.
Kocha huyo amejiunga na kikosi hicho na kukiongoza katika michezo 10 na ameshinda sita, sare miwili na kupoteza pia miwili, akichukua nafasi ya Maka Mwalwisi aliyejiunga na Mbeya Kwanza, aliyeiongoza mechi 15 za msimu huu.
Timu hiyo inayopigania nafasi nne za juu, inashika nafasi ya sita na pointi 48, baada ya kushinda michezo 14, sare sita na kupoteza pia sita kati ya 26, huku safu ya ushambuliaji ikifunga mabao 36 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara 23.