
Anti naomba unishauri bila kunificha. Ninatafuta mwanaume wa kuzaa naye tu, mtoto nitalea mwenyewe. Ninafanya hivyo kwa sababu wanaume wanasumbua sana,ukizaa naye kisha ukamtegemea anakuletea makelele mengi wakati ambao mtoto ameshamjua baba yake unashindwa kutengana au kukaa mbali naye na kulazimika kuwa mtumwa wa kusikiliza karaha zake.
Hilo silitaki ndiyo maana nataka nipate mwanaume akinipa ujauzito tu iwe imeishia hapo, nijipatie mtoto wangu maisha mengine yaendelee. Naomba nisaidie kujua nitapata wapi mwanaume wa aina hiyo? Pia nipe mtazamo wako katika uamuzi wangu huu.
Acha kabisa kufikiria mambo yasiyokuwa na matokeo chanya kwenye jamii. Nakubaliana na wewe sehemu moja tu ya kuzaa huku ukijipanga kulea mtoto mwenyewe kwa sababu kuwa na baba haikuondolei wewe kama mama nafasi ya kumtunza mwanao. Ila kina baba msininukuu vibaya, jukumu la kutunza familia ni lenu kwa asilimia 100.
Nirudi kwenye suala lako la msingi katika jamii nyingi za Kiafrika, mwanaume na mwanamke wanaposhirikiana kuleta mtoto duniani, wanatarajiwa kuwa wazazi wawili wenye jukumu la pamoja katika malezi ya mtoto.
Mpango wa kuzaa kisha kuwa na mtoto wako peke yako bila kumuonyesha mtoto baba yake wala kushirikiana naye katika malezi kisa kina baba wanasumbua na wana makelele mengi, siuoni kama ni sahihi kabisa.
Kwako unaweza kuuona una faida kadhaa, lakini kiuhalisia una athari nyingi kwa mtoto, hasa katika suala la malezi, kisaikolojia na mtazamo wa kiutamaduni.
Kwanza, kukosa malezi ya baba kunaweza kumkatisha tamaa mtoto. Watoto wanahitaji malezi kutoka kwa wazazi wote wawili ili kukua vizuri katika mazingira yenye usawa wa kihisia na kijamii.
Unaweza kusema baba yake akifariki je, hilo ni suala jingine. Baba anachangia katika kutoa mfano wa jinsi mwanaume anavyopaswa kuwa, na pia humsaidia mtoto kuelewa tofauti kati ya jinsi na majukumu yao katika jamii.
Hali hii ya kukosa baba inaweza kumfanya mtoto ajisikie mpweke na wa tofauti miongoni mwa wenzake anaweza hata kuchanganyikiwa, au kuwa na maswali yasiyo na majibu kuhusu alipo baba yake.
Katika mazingira haya, mtoto huenda akajikuta akilazimika kuunda picha ya baba mbadala katika mawazo yake, jambo ambalo linaweza kuathiri sana ukuaji wake wa kisaikolojia.
Aidha, athari za kisaikolojia ni kubwa. Mtoto anapokosa malezi ya baba mara nyingi anaweza kukumbwa na hisia za kukataliwa na kukosa usahihi wa yeye ni nani hasa, asili yake ni ipi na kwa nini yupo tofauti na wengine.
Tunapoangazia matatizo ya kihisia kama vile huzuni, wasiwasi, au hata hasira, tunaona kuwa maisha ya mtoto yanaweza kuwa na changamoto nyingi kuliko wale wanaokua na wazazi wawili.
Ukubwani huyu mtoto anaweza kuwa na tatizo la kutojenga uhusiano mzuri na wengine. Hapa litazaliwa tatizo jipya la kushindwa kumudu changamoto katika jamii inayomzunguka, anaweza kuwa mbinafsi pia, kwani hana la kupoteza na anaamini alitengwa tangu mdogo.
Mbali na athari za kisaikolojia, kuna mtazamo wa utamaduni ambao haupaswi kupuuzwa hata kidogo Katika utamaduni wa Kiafrika, baba anachukuliwa kuwa nguzo muhimu katika malezi ya mtoto. Wanaume wanategemewa kutoa usalama, ulinzi, na muongozo wa kimaadili.
Kukosa baba, kwa hivyo, sio tu kumwondolea mtoto mzazi mmoja, bali pia kunampokonya mtoto maadili na mizizi ya kitamaduni ambayo ni muhimu kwa ukuaji wake.
Katika utamaduni wa Kiafrika, kila mtoto anahitaji baba ili kukamilisha familia na kuweza kujiunga na jamii kwa njia sahihi.
Kukosekana kwa baba kunaweza kuleta mabadiliko makubwa katika tamaduni na desturi za familia, na hivyo kuwa na athari nyingi kwa jamii kwa ujumla.
Kwa ujumla wazo lako lina faida chache sana ikiwamo kujiepusha na karaha za wanaume kama ulivyojenga hoja ya wazo hilo, lakini athari ni nyingi zaidi hasa kwa mtoto.
Ingawa ni hiari yako kuchagua ni namna gani unapanga kuzaa na kumlea mwanao, lakini athari zinazoweza kumkabili mtoto ni tofauti na matarajio yako. Kutokana na yote hayo, sikushauri kuzaa mtoto na kumlea katika malezi hayo labda kuwe na changamoto nyingine.
Pia nakushauri tafuta mwenza utakayefanya naye maisha kihalali achana na hili wazo la kutafuta mtu tu uzae naye, hili jambo limekaa Kimagharibi sana, huu si utamaduni wetu Waafrika. Jamii haitokuelewa.