Heri ndoa za zamani zilizodumu kuliko…

Siku hizi, ndoa zinafungwa na kuvunjika sana. Tofauti na zama zile, zamani, mababu na mabibi walirahisishia mambo na kujengea misingi imara ya ndoa tofauti na sasa.

Hawakubeba mashada ya maua wala kwenda fungate. Hawakukodisha kumbi wala magari ya bei mbaya. Tofauti, walibeba uaminifu na uvumilivu vitu ambavyo ni ghali wakati huu.

Hawakuvishana pete za fedha wala dhahabu. Hawakuvaa suti wala shela lakini bado walioana wakatutuza japo baadaye tuliwaona na kuwaita waliopitwa na wakati!

Nani kapitwa na wakati kati yao nasi tusiojua hata wakati ni nini kiasi cha kuupoteza tena kwenye ujinga na uovyo?

Ama kweli shukrani ya punda ni mateke. Je, pamoja na usasa wetu wao na ukale wao, hatuongozi njia kwenda kwenye maangamizi yetu ambayo yamekuwa chanzo kikubwa cha mmomonyoko wa maadili?

Zamani, wachumba hawakuchagua mali bali utu. Hawakuchagua wala vyeo bali maisha. Nani alizaliwa na mali? Wengi  wanaotaka wachumba matajiri ni watoto wa maskini tena wa kunuka.

Ni wezi wasiotumia silaha zaidi ya miili yao. Watakao wenye vyeo vikubwa si wao wala wazazi wao wenye navyo.

Huu ni wizi japo hauitwi hivyo. Kama mali na madaraka ni vigezo vya kupata akufaaye, mbona wazazi wako walifunga ndoa na kukuzaa wewe wakiwa maskini wa kunuka?

Wangapi wameolewa na majambazi na wauza mihadarati hata wauaji kwa vile wana mali wakaishia kujuta na wengine kuuawa? Tia akili wewe utakaye mchumba akufaaye.

Hapa kuna shurti. Ili akufae, nawe shurti umfae kisha mfaane. Ndoa si mali. Ni zaidi ya mali. Ni hifadhi yako. Siyo chimbo la fedha wala utajiri.

Heri mume maskini akupendaye kuliko tajiri anayekudharau na kukuona kama sehemu ya mali yake. Nani anakithamini kiatu hata akinunue kwa milioni?

Bibi zetu hawakuvaa sidiria ili maziwa yao yaonekane bado yamo japo yalianguka zamani. Ya nini iwapo kuzaa na kunyonyesha ilikuwa heshima na jambo la kujivunia?

Je, maziwa siyo haki ya mtoto? Nani atabaki mrembo daima kama siyo kujihadaa ukajiridhisha na kudhani unawahadaa wengine?

Kina bibi wavae sidiria ili wamvutie nani? Bibi na babu hata mama na baba hawakukata keki siku ya harusi yao. Walibarikiwa na kushikana mikono na kujinywea pombe.

Je, haya siyo matunda ya amani na utulivu wao? Wala hawakwenda kanisani kuimbiwa na kupigiwa hoi hoi, vifijo, na vigelegele.

Kwao Mungu alikuwa kila mahali. Wangeendaje kanisani wakati kanisa lilikuwa nyoyo zao? Wala hawakula viapo. Wangeapia nini iwapo walikuwa wakipendana kweli kweli bila kujali alichokuwa nacho mtu zaidi ya utu wake?

Leo, tunalishana viapo. Kesho tunavivunja na kutimuana kwa kashfa na aibu. Wengine wanafikia kutoana roho. Wanafanya yote haya bila kujua hasara zake.

Ajabu, bado wanasema ni usasa wakati ni kuvunjika mioyo! Wangapi wamejifilisi ili wagharimie ndoa na wasifike? Nani aweza kula sifa? Nani anaichukia jana iwapo leo yake ni mazabe matupu?

Tusionekane twazusha. Angalia idadi ya ndoa zinazovunjika na jinsi wanandoa wanavyodhalilishana na kuumizana siku hizi. Tatizo ni nini? Waja wamekumbatia vitu hadi kuvigeuza ibada.

Zamani, hapakuwapo na nyumba ndogo wala kubwa. Nyumba ilikuwapo moja. Japo hawakuwa malaika, japo watu walikuwa wakweli. Walioa na kuolewa mitala bila kificho na unafiki. 

Japo hatupendi wala kuunga mkono mitala, heri ya mitala wazi kuliko ukahaba fiche hata ukipewa majina mazuri vipi.

Pamoja na kuonekana kupitwa na wakati, ndoa za mababu zetu zilidumu, wakati za kisasa nyingi ni talaka tarajiwa!

Zamani, vijana walikwenda jandoni na unyagoni kufundwa wajue maana ya ndoa. Siku hizi, taasisi hizi zinaonekana jambo lililopitwa na wakati! Nani anaweza kushindana na wakati usimuache?

Hivi waliopitwa na wakati ni wao au sisi tunaougulia mavuno na mateso ya miigizo ya mila za wenzetu? Tunamwagiana ‘champagne’. Hiyo Champagne mnayojivunia mwajua inatengenezwa wapi? Mnajua ni pesa gani mnaharibu tena kwa kuibiwa na hao waliowaletea utamaduni huu ili wawaibie muwe maskini wao watajirike?

Heri kuvaa shela ya roho ukafika mwisho wa safari kuliko ya mwili ukaikatiza safari. Je,  umejifunza nini kuhusiana na ndoa na wakati? Unaweza kwenda nyuma, ukadhani unakwenda mbele. Heri ndoa za zamani zilizodumu kuliko za sasa zinazovunjika kirahisi. Hilo ndilo somo la leo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *