Wanaume sasa vinara wa umbea!

Huko nyuma ukisikia msamiati umbea harakaharaka akili ilikuwa inakupeleka kwa wanawake.

Kutokana na asili yao si aghalabu kukuta kiumbe wa jinsi hii akiwa na uwezo mkubwa wa kuhifadhi mambo kifuani.

Ikitokea sasa kushindwa kwake kuhifadhi akayapeleka sehemu kusikostahili msuto unamhusu, hivyo umbea ulikuwa ukifanyika kwa siri na tahadhari kubwa kukwepa fedheha.

Katika ulimwengu huu wa kidijitali mambo yamebadilika umbea unafanywa hadharani na mtu anaona ufahari kutambulika kwamba yeye ni mmbea.

Bahati mbaya zaidi wanaume nao wameingia kwenye hili tena kwa kasi kuliko hata hao wanawake.

Nakumbuka Rais Samia Suluhu Hassan katika moja ya mahojiano yake aliyowahi kufanya na chombo cha habari wakati huo akiwa Makamu wa Rais aliwahi kusema: “Nasikitika kusema siku wanaume ni wambea zaidi tena kuliko wanawake.’’

Kinachoendelea kwenye mitandao ya kijamii kwa sasa kuhusu madai ya kuvunjika kwa ndoa ya Haji Manara ni kipimo tosha kwamba tuna jamii inayoendekeza umbea, watu wameacha shughuli zao wanahaingaika kufuatilia kila kinachoendelea.

Hapa inahusisha wanawake kwa wanaume huku kukiwepo watu walioamua kujitangaza hadharani kwamba hiyo ndiyo biashara yao, yaani mtu anaona sifa kabisa kusimama kifua mbele kueleza kwamba kufuatilia maisha ya watu ndio kunamuweka mjini.

Wapo ambao tayari wameshajitengenezea chapa kwamba wao ndiyo wambea maamuru, kiukweli inasikitisha, kijana shababi ambaye alipaswa kuwa na mchango mkubwa kwenye ujenzi wa Taifa anajigamba kwamba yeye ni mmbea wa Taifa  

Hayo yanasababisha siku hizi watu kutumia  muda mwingi kutafuta umbea na taarifa binafsi za watu wengine kuliko kutafuta maarifa. Yaani kutaka kujua fulani anaishije, analeaje watoto, ndoa yake inaendeleaje, wataachana lini na yapi anayopitia baada ya ndoa yake kuvunjika.

Haya yote yanafanywa na wanawake na wanaume, unakuta mtu ni heri akose vitu vyote lakini sio kifurushi cha intaneti kwenye simu yake kitakachomuwezesha kuingia mtandaoni kupata habari.

Mtu yuko radhi akeshe hadi usiku wa manane akisubiri taarifa za umbea zilizoahidiwa kuwekwa hadharani na mmbea mmoja aliyezinasa, halafu unakuta anayefanya hivi ni mwanaume, yaani mwanaume ameamua na kujitangaza wazi wazi kwamba hakuna namna utamtenganisha na umbea.

Binafsi nasikitishwa na mwenendo huu, kwa sababu kama ambavyo tumetengeneza kizazi cha machawa,chenye kazi ya kusifia tu naona hili la umbea nalo ni tatizo kubwa na lisipotafutiwa dawa itakuwa ajira kama ilivyo kwa uchawa.

Siku hizi vijana wameamua wasihangaike kutafuta ajira, wamejiajiri kwenye kusifia viongozi na watu wenye pesa.

Kwa kufanya hivyo wanajipatia chochote kitu na mkono unaenda kinywani.

Sasa wale wasiokuwa na uwezo wa kuwafikia viongozi au watu wenye fedha ndiyo hawa wanashinda mitandaoni kutafuta kujua nani kafanya nini na anaendeleaje na mbaya zaidi kuwatolea maneno ya ovyo yenye kukatisha tamaa au kuongeza maumivu.

Nakerwa na haya kwa sababu tunatengeneza kizazi cha ovyo mno, watoto wanayaona yanayofanyika na wanajifunza kile wanachokiona, akiona mama au baba yake ni kinara wa kufuatilia maisha ya watu na sio kufanya kazi kwa jasho hata yeye atakua akiamini kwamba hayo ndiyo maisha.

Katika hili, msisitizo wangu tusimame kwenye misingi ya kufanya kazi, kujua fulani kinaendelea nini kwenye maisha yake haiwezi kukusaidia chochote kwenye maisha yako zaidi ya kukupotezea muda wa kufanya yako.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *