
Kuna siri ambayo wanaume wanaodharau na kutesa wake wao hawajui.
Siri hii ni kuwa wanawake wanachangia kwa kiasi kikubwa katika ufanisi wa waume wao. Wanaume wengi waliofaulu na kuwa na mali na familia thabiti, huwa wanahusisha ufanisi wao na mchango wa wake zao.
Mwanamume asiyeheshimu mkewe ni sawa na bure.
Hawa ni wale wanaume waliotekwa na kuganda katika itikadi zilizopitwa na wakati ambazo wanawake walichukuliwa kama vyombo vya kutumiwa na wanaume na kuwazalia watoto.
“Inasikitisha kwamba hata katika karne hii, wapo wanaume katika baadhi ya jamii wanaochukulia wanawake kama viumbe duni na kuwataka kupiga magoti mbele yao kuwatii hata wakati haki zao za kimsingi zinakiukwa,” anasema mshauri wa wanandoa Janet Mbii.
Wanaume kama hao, asema, wanafaa kupatiwa mafunzo watambue kuwa mwanamke anapoheshimiwa, hurudisha heshima hiyo maradufu kwa mumewe na anapodharauliwa, huwa analipiza kwa dharau pia.
“Mume anayewezesha mkewe kwa hali yoyote ile, huwa anavuna matunda ya maisha yenye amani, mapenzi tele na familia thabiti. Kazi ya mwanamke si kupikia mumewe na kumtandikia kitanda kisha ampashe joto. Mwanamke ana haki ya kuheshimiwa na kuruhusiwa kutoa maoni yake katika ndoa sio kuwa mtumwa wa mumewe na jamii jinsi baadhi ya watu wanavyowachukulia,” anasema.
Katika ulimwengu wa kisasa ambao wanawake wanapata elimu sawa na wanaume, maoni yao hayafai kuchukuliwa kuwa duni.
“Baadhi ya wanaume huwa wanakosea kwa kuendesha udikteta katika ndoa kwa kutawaliwa na imani potovu za kijamii na kidini kuwa wake wao wanapaswa kukubali kila wanachotaka wafanye na hawafai kutoa sauti mbele yao,” anasema.
Kwa upande wake, Patrick Siacho, mwanasaikolojia na mshauri wa masuala ya ndoa, anasema: “Huu ni ukandamizaji unaonyima mwanamume nguzo muhimu sio tu ya ufanisi wake bali pia furaha yake. Ukweli mchungu ni kwamba mke wa mtu ni wake peke yake na sio wa jamii kama baadhi ya wanaume wanavyosisitiza kama kisingizio cha kuwadharau wake wao.”
Anasema enzi za wanaume kutisha wanawake kwa kusingizia desturi za jamii zimepitwa na wakati huku wanawake wakiendelea kusoma na kufunguka macho.
“Kufunguka macho kwa wanawake, kunafuta dhana kwamba ni viumbe wa kufungwa nyumbani, wasio na uhuru wao wa kujumuika na marafiki kwa shughuli za kijamii, kiuchumi na kisiasa. Mwanamume asiyemhusisha mkewe katika mipango yake huwa amepoteza mwelekeo kabisa na kuwa kama kipofu,” asema Siacho.
Mtazamo wa dini
Mchungaji wa Kanisa la Pentecostal Evangelistic Fellowship of Africa (PEFA) Wilaya ya Rorya mkoani Mara, Gerald Noah anasema nafasi ya mume kiimani ni kusimamia na kulinda familia huku ya mke ikiwa ni kutunza familia.
“Mume anahakikisha familia yake ina afya nzuri, inapata haki za msingi ikiwemo watoto kusoma, wanalala vizuri, wanakula vizuri, wanavaa vizuri lakini mke anatakiwa kuangalia ustawi wa watoto wake na mume wake. Lakini muhimu zaidi wote nafasi yao kubwa ndani ya ndoa ni kuhakikisha kila mmoja anatimiza haki ya mwenziwe ya tendo la ndoa,”anasema.
Anaeleza kuwa kiimani kuna kipengele kinasema mke anapokosea aonywe kwa upole au hata kwa kukaripiwa.
“Kuna watu wanafikiria kuonya ni kupiga na wengine wanapenda kukaripia lakini kukaripia ni pale umeshasema kwamba hiki kitu sikitaki, lakini kinaendelea kufanyika hivyo unasisitiza ndio maana tunaambiwa tuonye kwa upole lakini kwa kukaripia,” anaeleza.
Naye, Shekh wa Mkoa wa Simiyu, Issa Kwezi anasema katika imani ya dini ya Kiislam, mume na mke kila mmoja ana nafasi yake.
“Yaani kila mmoja kawekwa kwenye wizara au idara yake, kwenye Quran ametajwa wanaume ndiyo wasimamizi juu ya wanawake kama ni uongozi, mwanaume ndiyo kiongozi wa familia ndiyo kawekwa pale. Na ndio maana Mtume ( Rehma na amani zimshukie) alisema kila mmoja ni mchunga na mchunga ataulizwa kutokana na mchunga wake…wa kwanza akawa ni mwanaume na mwanaume ni mchunga juu ya familia yake lakini mwanamke pia akaambiwa na yeye ni mchunga juu ya watu wake wakiwamo watoto, watumishi wa nyumbani, kuna mali zinazozunguka familia hizo zipo chini ya mwanamke,”anafafanua.
Kuhusu adhabu kwa mke, anasema katika Uislamu adhabu zipo, lakini ni hatua ya mwisho baada ya usuluhishi ukiwamo wa wazazi.
“Kwenye Uislamu tumeambiwa tuchukue hatua na hatua ya kwanza ukiona mambo hayaendi ndani unawaita upande wa mkeo na upande wako mwanaume mnakaa chini mnasinulia matatizo yenu.Wao wanakuwa wasuluhishi ikionekana matatizo hayaishi pamoja na kuchukua hiyo hatua sasa ndiyo unaingia kwenye adhabu, ” anasema na kuongeza:
“Na adhabu zimetajwa kwa utaratibu. Jambo la kwanza umuonye kwa kumwambia tabia unayoendelea nayo mimi naona haifai kama unaona anaendelea pamoja na kumuonya tumeambiwa tutoe adhabu ya kumhama kitanda abaki peke yake kwa muda utakaoona unafaa…kuna watu wengine unakuta ana mke zaidi ya mmoja anahamia moja kwa moja kwa mwanamke mwingine kama kuhama kitanda haijasaidia imezungumzwa adhabu ya kipigo kisicho na madhara.”
Saikolojia
Mtaalamu wa masuala ya saikojia ya maisha na uhusiano, Mwalimu Yatabu anasema kuna madhara ya kisaikolojia na kimwili endapo mwanamke atakuwa akinyanyaswa au kudharauliwa na mume wake au ndugu wa karibu ikiwemo kupata hali ya kuweweseka na msongo wa mawazo.
“Mwanamke anapokuwa ananyanyasika kwa maneno au vitendo, inamsababishia kutojiamini, kupoteza ujasiri na kupoteza ladha sahihi ya maisha. Kitu kingine husababisha msongo wa mawazo kwa sababu anapokuwa anaishi sehemu ambayo hakuna amani, anakosa furaha, anakosa ile hali aliyotarajia kuiona…” anasema.
Anasema kiakili pia kuna hatari ya kupata magonjwa ya afya ya akili, wasiwasi kupita kiasi, sonona na magonjwa mengine ya akili, akieleza ubongo unapopata tatizo au jambo linalosababisha kichwa kisifanye kazi ipasavyo anapoteza hamu ya kuishi.
“Ndio maana tunaona baadhi ya wanawake wanakuwa wakatili kwa watoto si kwa sababu watoto sio wao ila ni kwasababu ya ukatili wanaofanyiwa na waume zao, yale yanamjenga mwanamke kuwa katika hali ya hatari. Yale maneno ambayo anaambiwa na mwanaume ni jambo analoishi nalo na linaenda linajenga chuki na sumu mwilini hata kichwani,”anaeleza Yatabu.
Anawashauri wanaume kuacha kutamka maneno yanayotweza utu kwa wenza wao.
” Haijalishi amekosea kiasi gani kwakuwa neno moja linaweza kusababisha madhara ikiwemo kupata wazo la kuua, kujiua au kujidhuru kwa sababu anakuwa ameshindwa kuuongoza ubongo wake,” anasema.