Mtoto asiyependwa nyumbani hawezi kupenda

Umewahi kufikiri namna tunavyoendelea kutengeneza kizazi cha watu wanaochoshwa na upendo?

Kuna ukweli mchungu kuwa tumeanza kuwa na kizazi cha watu wasiojali uhusiano wala hisia za watu.  

Hiki ni kizazi, aghalabu, kilichozaliwa na kizazi cha wazazi wasomi, wenye pesa kuliko kizazi kilichopita.

Ukweli mchungu ni kwamba tunaishi kwenye nyakati ambazo wazazi hatuna muda wa kupenda kupatikana kihisia, kuzungumza, kusikiliza, kuhusiana, kujali na kadhalika.

Badala ya kupenda, kwa maana ya kupatikana kihisia, kuzungumza na kujali tunatumia vitu kuziba ombwe.

Tuna kizazi kipya cha wazazi wanaothamini vitu kuliko kitu kingine chochote. Tunatumia muda mwingi kazini, kwenye biashara, na shughuli nyingine za kutafuta vitu. Na kweli wazazi wengi wa sasa wanavyo vingi kwa maana ya vitu na penda kuliko vile walivyokuwanavyo wazee wetu.

Bahati mbaya sana wingi huu wa vitu na pesa unakuja na gharama kubwa ya kutopatikana. Hatuna muda wa kuhusiana na watoto.

 Kwa vile hatuna muda wa kupatikana, tunatumia vitu vingine kama  nyenzo muhimu ya malezi. Katika kufunika hatia ya kutopatikana, tunawahonga watoto midoli wasiyoihitaji.

Mtoto akilia, kwa mfano, tunampa kishikwambi atulie. Nyumba zetu zina kila aina ya ving’amuzi vinavyotumiwa muda mwingi na watoto wetu. Katuni zinatumika kupotezea hitaji la mtoto kusikika na kuonekana.

Tukishindwa kuzungumza na mtoto tunawasha runinga kumnyamazisha. Tukikosa muda wa kulea tunalipia chekechea ya bweni.

Unaweza kuona ongezeko la wimbi la watoto wadogo ambao kimsingi bado wana utegemezi mkubwa kwa wazazi kupelekwa shule za bweni.

Kwa mazingira haya, mtoto anaanza kujifunza namna mpya ya kushughulikia mahitaji yake ya kihisia kwa ugumu na maumivu makubwa. Watoto wengi, mathalani, wamejifunza kuishi maisha ya upweke.

Hawana uhusiano wa karibu na wazazi wao. Ukimuuliza mtoto leo nani anamwamini zaidi, nani anaweza kumwambia hofu zake, mambo yake binafsi, unaweza kushangaa anayetajwa ni mtu mwingine nje ya familia aghalabu anayeonekana zaidi kwenye runinga.

Tunafahamu mzazi ndiye mwenye mchango mkubwa kujenga dhana ya kipi ni muhimu zaidi kwa mtoto

Kupitia matarajio anayoyaona kwa mzazi wake, mtoto anajifunza nini hasa ni cha muhimu kwa mzazi wake. Mtoto anajua, kwa mfano, kilicho muhimu kwa mzazi ni matokeo.

Kila anapokutana na mzazi swali la maana analoulizwa ni matokeo. Ugomvi mkubwa ni matokeo. Ukitaka kumfurahisha mzazi faulu mengine yote ikiwemo maadili yanavumilika.

Muda na nguvu nyingi zinatumika kupuuza hisia zake. Upweke, kupuuza hisia, kucheza na hisia za watu, ubinafsi, kukweza vitu na wenye vitu inakuwa sehemu ya uhusiano.

Mtazamo huu wa maisha unaunda mwelekeo mpya wa uhusiano na watu ili kumudu uhaba mkubwa wa upendo.

Rejea aya ya kwanza kwa tafsiri ya upendo. Matokeo yake, tukifikia umri wa uhusiano, tunachoshwa haraka uhusiano unaotudai tupende.

Tunataka kupendwa lakini hatuelewi upendo maana yake nini. Tunataka kuaminiwa lakini tunamchoka haraka anayetuamini. Hatujazoea kuaminiwa.

Tunatamani kueleweka lakini tunatishwa na muunganiko wa hisia. Tumezoeshwa vitu kutumika kama mbadala wa kuhafahamiana vizuri, kuunganika kihisia na shauku ya kuwa karibu na mtu.

Tunalea kizazi ambacho ukimnyima mtu muda wako ukampa pesa anaamini unampenda, hata kama utamuondoa kabisa kwenye ratiba zako. Ukimpa mtu muda wako, usikivu, ukawekeza kwenye uhusiano, lakini usiwe na pesa mtu anaona unamchosha.

Ukimnyima muunganiko wa hisia, ukampa uhakika wa ufundi wa ngono anachagua ngono hata akikosa uhakika wa uhusiano wa kudumu. Jitihada zozote za kudumisha uhusiano bila ngono inaonekana ni mzaha na ndoto za abunuwasi.

Hatutaki kuwekeza tunataka kupita. Hatutaki kudumisha tunataka kusisimka. Hatutaki kufahamiana tunataka kutumiana.

Hatutaki kujipa muda tunataka kilicho tayari. Hatutaki gharama tunataka matokeo. Hatutaki kutafuta tunataka vya kupewa.

Hatutaki kusubiri tunataka ghafla. Hatutaki uaminifu tunataka uhuru. Hatutaki usisi tunataka umimi.

Hiki ndicho kizazi kinachoishi matokeo halisi ya utoto uliotelekezwa. Mtoto asiyependwa nyumbani hawezi kupenda.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *