Mwili wa mwanamke wakutwa nje ya nyumba ukiwa mtupu

Unguja. Mwili wa mwanamke ambaye bado hajafahamika jina, umekutwa leo Aprili 12, 2025, saa 12 asubuhi nje ya jengo la Michenzani, Block namba nane, katika Mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, ACP Abubakar Khamis Ally amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa uchunguzi wa awali umeonyesha kuwa mwanamke huyo alikuwa tayari amefariki dunia wakati mwili wake ulipogundulika.

“Hadi sasa hatujambaini utambulisho wake jina, makazi wala umri. Mwili huo umepelekwa katika Hospitali ya Mnazimmoja kwa uchunguzi zaidi ili kubaini chanzo halisi cha kifo,” amesema Kamanda Ally.

Sheha wa Mwembetanga, Ramadhan Omar amesema alipokea taarifa hizo kutoka kwa mkazi wa eneo hilo aliyemuambia kuwa kuna mtu amelala chini ya ngazi na hali yake haikuwa ikieleweka.

“Nilipofika katika eneo hilo, nilikuta tayari baadhi ya wasamaria wema walikuwa wamemfunika kwa nguo, kwani mwili wake ulikuwa bila nguo kabisa,” amesema sheha huyo.

Ameongeza kuwa alitekeleza wajibu wake kwa kuwajulisha vyombo husika mara moja ili hatua zaidi zichukuliwe.

Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi ili kubaini utambulisho wa marehemu na chanzo cha kifo chake. Wananchi wanahimizwa kushirikiana na vyombo vya usalama kwa kutoa taarifa yoyote itakayosaidia kufanikisha uchunguzi huo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *