Man City yatoa dozi ikiishusha Chelsea EPL

England. Manchester City imepanda hadi nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu England (EPL) baada ya kuibuka na ushindi mnono wa mabao 5-2 dhidi ya Crystal Palace kwenye Uwanja wa Etihad, Manchester leo Jumamosi, Aprili 12, 2025.

Pamoja na Crystal Palace kutangulia kwa mabao mawili, Man City ilionyesha kiwango bora na kusawazisha mabao hayo kisha kuongeza mengine matatu yaliyoifanya imalize kibabe mechi hiyo.

Ebelechi Eze alianza kuifungia mapema Palace katika dakika ya nane akimalizia pasi ya Pape Sarr na dakika ya 21, Chris Richards aliongeza bao la pili akimalizia pasi ya Adam Wharton.

Manchester City ilijibu kwa haraka mabao hayo kupitia kwa Kevin De Bruyne katika dakika ya 33 na baadaye Omar Marmoush katika dakika ya 36 na hadi filimbi ya mapumziko inapulizwa, matokeo yalikuwa sare ya mabao 2-2.

Kipindi cha pili ndio kilikuwa kigumu zaidi kwa Crystal Palace kwani City ilifunga mengine matatu kupitia kwa Mateo Kovacic (dk 47), James McAtee (dk 56) na Nico O’Reilly (dk 79).

Ushindi huo umeifanya Manchester City kufikisha pointi 55 na kupanda hadi nafasi ya nne ikizipiku Chelsea na Newcastle United.

Bao la Kevin de Bruyne limemfanya nyota huyo wa Ubelgiji kuwa mchezaji wa sita kufunga mabao 30 au zaidi akiwa nje ya eneo la hatari katika Ligi Kuu England.

Hii ni mara ya tatu kwa timu kuibuka na ushindi wa tofauti ya mabao matatu baada ya kutanguliwa kwa mabao mawili na Manchester City imefuata nyayo za Arsenal iliyofanya hivyo dhidi ya Tottenham Hotspur mwaka 2012 na Manchester United iliyofanya hivyo dhidi ya Spurs mwaka 2009.

Manchester City imeboresha rekodi yake ya kufunga mabao matano au zaidi katika mchezo mmoja wa EPL mara  nyingi zaidi ambapo sasa imefanya hivyo mara 63 tofauti  ikiwa ni mara tano zaidi ya timu nyingine zilizowahi kufanya hivyo na kati ya mara hizo 63, mara 39 imefanya ikiwa chini ya Pep Guardiola.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *