
Dar es Salaam. Mtibwa Sugar inahitaji pointi nne tu katika mechi zake nne ilizobakiza kwenye Ligi ya Championship baada ya leo kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 mbele ya Mbuni FC katika Uwanja wa Manungui Complex, Morogoro.
Mabao ya Mtibwa Sugar leo yamepachikwa na Erick Kyaruzi na Omary Marungu huku lile la Mbuni likipachikwa na Thomas Malulu.
Matokeo hayo yameifanya Mtibwa Sugar kufikisha pointi 63 na hivyo kuifanya ihitaji pointi nne ili ifkishe pointi 67 ambazo zitaihakikishia kumaliza katika nafasi mbili za juu kwenye msimamo wa Championship ili ipande Ligi Kuu msimu ujao.
Upo pia uwezekano kwa Mtibwa Sugar kupanda Ligi Kuu ikiwa itashinda mchezo unaofuata dhidi ya Mbeya Kwanza na timu za Stand United na Geita Gold zikashindwa kupata ushindi katika mechi zao.
Katika raundi inayofuata, Geita Gold itakuwa nyumbani kuikaribisha Songea United huku Stand United yenyewe ikiikaribisha Green Warriors.
Kwenye Uwanja wa Mabatini, Mlandizi Pwani, wenyeji Green Warriors waliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Geita Gold, matokeo ambayo hapana shaka yamepokelewa kwa furaha na Mtibwa Sugar, Mbeya City na Stand United ambazo zipo kileleni mwa msimamo wa ligi.
Kichapo hicho cha leo kutoka kwa Green Warriors kimeifanya Geita Gold kubaki katika nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi ya Championship ikiwa na pointi zake 51, ikizidiwa kwa pointi 12 na Mtibwa Sugar inayoongoza, ikiachwa kwa pointi tano na Mbeya City iliyo nafasi ya pili ikiwa na pointi 56 na imeachwa kwa pointi nne na Stand United yenye pointi 55 ikiwa nafasi ya tatu.
Green Warriors kwa kuifunga Geita Gold leo, imepanda kwa nafasi moja hadi nafasi ya 11 kwenye msimamo wa ligi ikifikisha pointi 23.
Vita ya kupanda ilipofikia na mechi zilizobaki kwa timu nne za juu
MTIBWA SUGAR-Pointi 63
-Mbeya Kwanza vs Mtibwa
-Bigman vs Mtibwa Sugar
Transit Camp vs Mtibwa Sugar
Mtibwa Sugar vs Kiluvya United
MBEYA CITY-Pointi 56
Polisi Tanzania vs Mbeya City
Geita Gold vs Mbeya City
Mbeya City vs Cosmopolitan
Mbeya City vs Green Warriors
STAND UNITED- Pointi 55
Stand United vs Green Warriors
Cosmopolitan vs Stand United
Polisi Tanzania vs Stand United
Stand United vs Geita Gold
GEITA GOLD- Pointi 51
Geita Gold vs Songea United
Geita Gold vs Mbeya City
Biashara United vs Geita Gold
Stand United vs Geita Gold