Lazaro aachiwa msala Coastal Union

COASTAL Union iko sokoni kusaka kocha mpya wa kikosi hicho kwa ajili ya msimu ujao kutokana na aliyekuwepo Joseph Lazaro kutokuwa na leseni yenye uwezo wa kuongoza timu, lakini kwa sasa ataendelea kuiongoza.

Kikosi hicho kwa sasa kipo chini ya Lazaro baada ya kutimuliwa kwa Juma Mwambusi ambaye alijiunga na Coastal Union Oktoba 23 mwaka jana akiiongoza katika mechi 16 ambapo hakufanya vizuri.

Tangu apewe kikosi hicho Lazaro imecheza mechi mbili dhidi ya Yanga na kufungwa bao 1-0 katika Uwanja wa KMC na kurejea nyumbani – tangu msimu huu uanze na kukutana na Singida Black Stars na kuifunga 2-1.

Wagosi hao wameanza kupata matumaini ya kusalia katika ligi msimu ujao, baada ya kupanda kutoka nafasi ya 13 katika msimamo na kushika ya 10.

Hadi sasa imecheza mechi 26, ikiwa na pointi 28,ikiwa imeshinda michezo sita,sare na kupoteza 10 kwa kila mmoja, huku ikisalia na mechi nne mkononi.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo Omary Ayoub alisema  Lazaro anafanya vizuri lakini lazima watafute kocha mpya kwani leseni yake haikidhi vigezo.

Alisema kuwa, amerejesha matumaini makubwa na kama wataendelea hivi, basi msimu utakuwa umewaacha salama, ila kocha mpya ni wa muhimu.

“Kocha mpya anatikiwa aje mapema ajue kipi cha kuongeza na kupunguza pia, huku Lazaro akiendelea kuishika timu kwa muda mpaka atakapokuja. Ni wazi kuwa kocha Lazaro, anaijua timu hiyo kuanzia msimu uliopita na hata mpaka sasa, ila leseni yake ndio hairuhusu kuongoza kikosi kinachoshiriki Ligi Kuu, nje na hapo yuko vizuri,” alisema.

Coastal iliyorejea kwenye Uwanja wa nyumbani wa Mkwakwani jijini Tanga na kuanza na mguu mzuri kwa kushinda mabao 2-1 dhidi ya Singida Black Stars, imebakiza mechi nne zikiwamo tatu za nyumbanui na moja ya ugenini ili kufunga msimu wa 2024-2025.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *