
STAND United ‘Chama la Wana’ imesema dakika 90 iliyoiangalia Yanga imeona ugumu ulipo ikieleza kuwa licha ya kuiheshimu lakini haitaingia uwanjani kinyonge.
Timu hiyo iliyowahi kutamba Ligi Kuu kabla ya kushuka misimu mitano nyuma inaikabili Yanga keshokutwa, Jumanne katika mchezo wa robo fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho.
Chama la Wana kwa sasa lipo Championship likishika nafasi ya tatu likiwa na pointi 49 (kabla ya mechi ya jana) dhidi ya Songea United mechi itakayopigwa Uwanja wa Songea, Ruvuma.
Mara ya mwisho timu hizo kukutana ilikuwa Januari 19, 2019 katika mchezo wa Ligi Kuu Bara ambapo Stand United ilishinda bao 1-0 likifungwa na Jacob Massawe kwenye Uwanja wa Kambarage Shinyanga.
Hata hivyo, katika michezo sita ya mwisho wapinzani hao kukutana, Yanga imeshinda mara nne ikifunga mabao 19, huku Chama la Wana likitakata miwili likifunga mabao manne.
Meneja wa timu hiyo, Fred Masai alisema wameifuatilia vizuri Yanga kwenye mechi dhidi ya Azam iliposhinda 2-1 na kubaini kuwa eneo la kiungo na ushambuliaji ni balaa, hivyo wamejua wapi pa kuwazuia.
Aliwataja baadhi ya mastaa tishio kikosini humo kuwa ni Maxi Nzengeli, Clatous Chama, Prince Dube na Clement Mzize akieleza kuwa benchi la ufundi limeshawapa angalizo mabeki kuwa makini na nyota hao.
“Tutaenda kwa heshima kwakuwa wametuzidi mbali ila hatutakuwa wanyonge, Yanga tulishakutana nao na kupata matokeo yote ikiwa ni ushindi, sare na kupoteza.”
“Tuliwaona dhidi ya Azam na tulibaini wapi tuongeze umakini. Kuna wachezaji wengi wa kiwango cha juu haswa upande wa ushambuliaji, kocha Juma Masoud aliwaambia mabeki wetu nini wafanye,” alisema Masai ambaye pia ni katibu mkuu akiongeza kuwa uongozi unafurahishwa na mwenendo wa timu katika Championship.