
Geita. Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita linawashikilia watu wawili kwa tuhuma za kujifanya maofisa polisi na kuchukua kiasi cha Sh25,000 kutoka kwa mwananchi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita Saphia Jongo amethibitisha kukamatwa kwa watu hao na kuwataja kuwa ni Ismail John (25) na Bosco John (28) ambaye ni dereva bodaboda wote wakazi wa Manispaa ya Geita.
Kamanda Jongo ameeleza kuwa vijana hao walikamatwa Aprili7, 2025 saa mbili usiku, katika Mtaa wa Samina, Kata ya Mtakuja Manispaa ya Geita, baada ya polisi kupata taarifa kutoka kwa wasamaria wema.
“Jeshi la Polisi lilipata taarifa za siri juu ya uwepo wa watu wawili ambao wamekuwa wakijifanya maofisa wa polisi wanawalaghai wananchi kisha kuwaibia fedha na mali zao kisha wanakimbia,” amesema RPC Jongo.
Amesema baada ya polisi kupata taarifa walishirikiana na wananchi na kuweka mtego uliofanikisha kukamatwa watuhumiwa hao, wakiwa katika mtaa huo wakifanya vitendo vya kihalifu, huku wakiwa wamepora Sh25,000 kwa mwananchi.
Kamanda Jongo amesema katika mahojiano na watuhumiwa hao wamekiri kujihusisha na vitendo vya kihalifu na kujifanya maofisa wa Jeshi la Polisi katika maneno mbalimbali ya Mkoa wa Geita.
Kwa mujibu wa Kamanda Jongo watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili baada ya taratibu za kisheria kukamilika.