Kaya abadilishiwa majukumu Singida Black Stars

Dar es Salaam. Makamu mwenyekiti wa Singida Black Stars, Omary Kaya ameteuliwa kuwa katibu mkuu wa klabu hiyo, mabadiliko ambayo yametangazwa rasmi leo Jumamosi, Aprili 12, 2025.

Taarifa iliyotolewa na Singida Black Stars, imeeleza kuwa kubadilishiwa majukumu kwa Kaya kumetokana na sifa alizonazo katika usimamizi na uongozi wa soka.

“Uongozi wa Klabu ya Singida Black Stars unayo furaha kuwataarifu mashabiki, wadau wa michezo na umma kwa ujumla kuwa, kuanzia tarehe 12/04/2025 Bodi ya Wakurugenzi imembadilishia majukumu na kumteua rasmi Omari Kaya kuwa Katibu Mkuu wa klabu yetu.

“Uteuzi huu umetokana na mchakato wa ndani uliozingatia sifa, uzoefu, na weledi katika masuala ya uongozi na usimamizi wa shughuli za klabu.

“Tunaomba ushirikiano kutoka kwa wadau wote ili aweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi na kuiwakilisha vyema klabu yetu,” imefafanua taarifa ya Singida Black Stars.

Kaya alijiunga na Singida Black Stars Oktoba 2024 ikiwa ni siku chache baada ya kuachana na Namungo FC ambayo yeye alikuwa akihudumu nafasi ya mtendaji mkuu.

Kabla ya kuitumikia Namungo FC, Kaya aliwahi kuhudumu ndani ya Yanga ambako alikuwa ni kaimu katibu mkuu.

Katika sekretariti ya Singida Black Stars, Kaya atafanya kazi sambamba na mtendaji mkuu wa klabu hiyo, Jonathan Kassano.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *