
Dodoma. Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Ramadhani Kailima amesema Chadema ambayo haikusaini kanuni za maadili ya uchaguzi, haitashiriki Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu na chaguzi zote ndogo zitakazofuata kwa muda wa miaka mitano.
Kanuni hizo zinasainiwa leo Aprili 12, 2025 na vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu, Serikali na (INEC) jijini Dodoma.
“Chama cha Chadema ambacho hakikusaini kanuni za maadili ya uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani wa mwaka 2025, hakitashiriki uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu na chaguzi zote ndogo zitakazofuata kwa muda wa miaka mitano.” amesema Kailima.
Awali, Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John Mnyika alisema haendi na hajatuma mwakilishi kwenda kusaini kanuni hizo.
Mnyika kupitia mtandao wa kijamii wa X na baadaye katika mazungumzo kwa simu na Mwananchi leo Aprili 12, 2025 amesema haendi na hajatuma mwakilishi kwenda Dodoma kusaini kanuni za maadili ya uchaguzi.
Alipoulizwa ni kwa nini hajateua mwakilishi Mnyika amesema: “Ni vyema mkaandika kwamba sijakwenda wala sijateua mtu. Habari kubwa sasa hivi ni katibu mkuu, sitakwenda kusaini wala sijateua mtu.”
Vyama ambavyo vimehudhuria hafla hiyo ni ADC, Demokrasia Makini, DP, NRA, NLD, SAU,UDPD, ADA- TADEA, AAFP, CCM, CUF, ACT-Wazalendo, CHAUMMA, UMD, TLP, NCCR-Mageuzi, CCK, UDP.
Kailima amesema kinachofuata sasa baada ya vyama vya siasa, Serikali na INEC kusaini kanuni hizo ni kwenda kuzichapisha kwenye Gazeti la Serikali.
“Utaratibu wa kusaini kanuni hizi ni leo tu hakutakuwa na siku nyingine kwa maana hiyo chama ambacho hakijasaini hakitaweza kushiriki uchaguzi na chaguzi nyingine ndogo zitakazofuata katika kipindi cha miaka mitano kwa sababu kanuni hizi uhai wake ni ndani ya miaka mitano kuanzia uchaguzi mkuu huu,” amesema.
Endelea kufuatilia Mwananchi.