Ajali ya helikopta yaua familia, rubani

New York. Familia ya watu watano kutoka Hispania imefariki dunia katika ajali ya helikopta ya utalii iliyotokea kwenye Mto Hudson, jijini New York, Alhamisi Aprili 10, 2025. Rubani wa helikopta hiyo pia amepoteza maisha.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Associated Press, waliopoteza maisha ni Agustin Escobar, mtendaji mkuu wa Kampuni ya Siemens Mobility ya Hispania, pamoja na mkewe Mercè Camprubí Montal, ambaye alikuwa meneja katika kampuni ya Siemens Energy. Watoto wao watatu, waliokuwa nao kwenye safari hiyo ya utalii, pia walipoteza maisha.

Picha zilizochapishwa kwenye tovuti ya kampuni inayomiliki helikopta hiyo zimeonyesha familia hiyo ikitabasamu muda mfupi kabla ya kupanda helikopta hiyo, tukio la furaha lililoishia kwenye majonzi.

Ilivyotokea

Safari hiyo ya utalii ilianza saa tisa alasiri kutoka kiwanja cha helikopta kilichopo katikati ya New York. Kwa mujibu wa rekodi za rada, helikopta hiyo ilielekea kaskazini ikipita juu ya mandhari ya Manhattan kabla ya kugeuza na kuelekea kusini, karibu na sanamu ya Uhuru, moja ya vivutio maarufu jijini humo.

Hata hivyo, ndani ya dakika 18 baada ya kuruka, helikopta hiyo ilipata hitilafu angani na kuanguka kwenye Mto Hudson karibu na New Jersey.

Video ya tukio hilo inaonyesha vipande vya helikopta vikiporomoka kutoka angani na kutua kwenye maji kwa kasi kubwa, ishara ya kuharibika kwa mfumo wa udhibiti angani kabla ya ajali hiyo kutokea.

Uchunguzi waendelea

Taarifa za awali zinaashiria uwezekano wa hitilafu kubwa ya kiufundi, ambayo huenda ilihusisha ‘rotor’ kuu ya helikopta ambayo ni sehemu muhimu ya kuinua ndege hiyo, kugonga sehemu ya mkia, na hivyo kuisambaratisha angani.

Mamlaka ya Usafiri wa Anga ya Marekani (FAA) pamoja na Bodi ya Kitaifa ya Usalama wa Usafiri (NTSB) zimeanza uchunguzi kubaini chanzo kamili cha ajali hiyo.

Meya wa jiji hilo, Eric Adams ameeleza kuwa vikosi vya uokoaji vilifanikiwa kuivuta helikopta hiyo kutoka mtoni saa mbili usiku kwa msaada wa kreni iliyobebwa na mtumbwi maalumu. Miili ya waliopoteza maisha ilipatikana ndani ya maji.

Kwa mujibu wa maofisa wa uokoaji, safari hiyo ilikuwa inaratibiwa na kampuni ya New York Helicopters. Hata hivyo, hakuna majibu yaliyopatikana kutoka ofisi za kampuni hiyo zilizoko New York na New Jersey.

Mtu aliyepokea simu nyumbani kwa mmiliki wa kampuni hiyo, Michael Roth, amekataa kuzungumzia suala hilo. Roth, katika mahojiano na New York Post, amesema kuwa ameshtushwa sana na ajali hiyo na hana taarifa kuhusu kilichosababisha tukio hilo.

“Kitu pekee nilichobaini kupitia video ya ajali ni kwamba rotor kuu haikuwa mahali pake kwenye helikopta.

 “Nimekuwa kwenye biashara hii kwa miaka 30, lakini sijawahi kuona jambo la aina hii. Hizi ni mashine, na huharibika.”

Mamlaka ya Usafiri wa Anga ya Marekani (FAA) imethibitisha kuwa helikopta hiyo ilikuwa ya aina ya Bell 206, mojawapo ya helikopta zinazotumika sana katika shughuli za kibiashara, utalii, polisi na vyombo vya habari. Hapo awali, ilibuniwa kwa ajili ya Jeshi la Marekani kabla ya kutumika kwa shughuli za kiraia.

Bodi ya Kitaifa ya Usalama wa Usafiri (NTSB) imetangaza kuwa itafanya uchunguzi wa kina kubaini chanzo halisi cha ajali hiyo.

Waliofariki ni kina nani?

Agustin Escobar, mmoja wa waliokufa, alikuwa mkurugenzi mtendaji wa kimataifa wa miundombinu ya reli katika kampuni ya Siemens Mobility na hivi karibuni aliteuliwa kuwa Rais wa Siemens nchini Hispania. Kulingana na akaunti yake ya LinkedIn, Escobar alifanya kazi Siemens kwa zaidi ya miaka 27.

Katika ujumbe wa shukrani kwa familia yake baada ya uteuzi wake mpya mwishoni mwa 2022, aliandika:

“Chanzo changu kisichokoma cha nguvu na furaha – kwa msaada wao wa dhati, upendo… na uvumilivu.”

Escobar alikuwa mstari wa mbele katika masuala ya uendelevu kwenye sekta ya reli na alisafiri mara kwa mara kwa kikazi, ikiwa ni pamoja na safari za hivi karibuni kwenda India na Uingereza. Tangu mwaka 2023, pia alikuwa makamu wa rais wa Chama cha Biashara cha Ujerumani nchini Hispania.

Maria Camprubí Montal, ambaye pia alifariki katika ajali hiyo, alikuwa mfanyakazi wa Siemens Energy huko Barcelona kwa miaka karibu saba, akiwa meneja wa biashara wa kimataifa na meneja wa kidijitali.

Maofisa wa Serikali ya kikanda ya Hispania walisema familia hiyo ilikuwa ikiishi Barcelona. Rais wa Mkoa wa Catalonia, Salvador Illa, aliandika katika mtandao wa X: “Nimesikitishwa sana na ajali ya helikopta kwenye Mto Hudson, New York, iliyogharimu maisha ya watu sita, watano kati yao wakiwa ni wa familia moja kutoka Barcelona.”

Rais wa Castilla-La Mancha, Emiliano García Page, aliongeza: “Agustín anatoka Puertollano, na mwaka 2023 tulimtangaza kuwa Mwana Mpendwa wa Castilla-La Mancha. Rambirambi zetu ziende kwa familia na wapendwa wake.”

Agali nyingine

Ajali ya Alhamisi ni ya kwanza kutokea Manhattan tangu ile ya mwaka 2019, ambapo helikopta iligonga paa la jengo refu na kumuua rubani.

Lakini anga la Manhattan limejaa shughuli za kila siku za ndege na helikopta. Tangu mwaka 1977, zaidi ya watu 38 wamepoteza maisha katika ajali za helikopta jijini New York.

Ajali kama ya mwaka 2009 ambapo helikopta ya utalii na ndege binafsi ziligongana juu ya Hudson, ziliua watu tisa. Mwaka 2018, watu watano walikufa baada ya helikopta ya kukodi kuanguka kwenye Mto East.

New York Helicopters pia inahusishwa na tukio la Juni 2013 ambapo helikopta nyingine aina ya Bell 206 ilipoteza nguvu na kutua kwa dharura kwenye Mto Hudson, ingawa abiria wanne hawakujeruhiwa.

Uchunguzi wa baadaye wa NTSB ulibaini kuwa hitilafu ya matengenezo na kasoro katika mfumo wa mafuta ya injini vilisababisha tukio hilo.

Ajali hizi zimeibua mjadala mkubwa kuhusu usalama wa safari za anga ndani ya miji mikuu kama New York. Wanaharakati na viongozi wa jamii wamependekeza kupunguzwa au kusitishwa kabisa kwa matumizi ya helikopta kibiashara ndani ya jiji hilo.

Hali ya tahadhari imezidi kuongezeka kutokana na matukio ya hivi karibuni, ikiwemo ajali ya ndege ya matibabu mjini Philadelphia mwezi Januari iliyoua watu saba, na ile ya ndege ya American Airlines kugongana angani na helikopta ya kijeshi mjini Washington siku mbili baadaye.

Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa mashirika ya habari.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *