
London. Meneja wa Arsenal, Mikel Arteta ametoa habari njema kwa mashabiki wa timu hiyo kuwa mshambuliaji wake Kai Havertz anaweza kurejea uwanjani kabla ya kumalizika kwa msimu huu.
Havertz alipata maumivu ya nyama za paja katika kambi ya Arsenal huko Dubai, Februari mwaka huu na baada ya hapo akafanyiwa upasuaji wa kuponya jeraha lake.
Majeraha ya Kai Havertz yamepelekea Arteta kumtumia kiungo Mikel Merino kama mshambuliaji wa kati wa timu hiyo kutokana na kumkosa pia Gabriel Jesus ambaye naye ni majeruhi.
Mwanzoni ilionekana kama Havertz atakosa mechi zote zilizosalia za Arsenal msimu huu lakini Arteta amefichua kuwa huenda wakawa naye katika mechi kadhaa za kumalizia msimu.
Matumaini ya Arteta yamekuja kufuatia kitendo cha mchezaji huyo kuanza mazoezi mepesi ya kumuweka sawa baada ya upasuaji aliofanyiwa.
“Historia kubwa ya jeraha, miiko ya hali ya juu ya kazi, ana hamu ya kurejea kucheza haraka iwezekanavyo na watu bora wa tiba wa kumtazama.
“Hivyo tuna matumaini tunaweza kuwa naye kabla ya mwisho wa msimu lakini acha tusubiri. Pale unapopata hatua ya mwisho ya kuimarika ndio unaweza kufahamu vizuri ukaribu au umbali utakaokuwa nao kwa hatua inayofuata,” amesema Arteta.
Hadi anapata majeraha, Havertz alikuwa amehusika na mabao 20 ya Arsenal katika mechi 34 za mashindano tofauti ambapo alikuwa amepachika mabao 15 na kupiga pasi tano za mwisho.
Ukiondoa mechi dhidi ya Brentford leo, Arsenal itabakiza mechi sita kwenye Ligi Kuu England (EPL) ambazo ni dhidi ya Ipswich, Crystal Palace, AFC Bournemouth, Liverpool, Newcastle United na Southampton.