Chadema kwenye mtego mwingine kanuni za maadili

Dar es Salaam. Tusaini au tusisaini? ndilo swali lisilo na jawabu ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kwa sasa, kuhusu ushiriki wake katika kujadili na kusaini Kanuni za Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani kesho Aprili 12, 2025.

Kanuni za maadili zimeandaliwa kwa mujibu wa kifungu cha 162 (1), (2) na (3) cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na. 1 ya Mwaka 2024 ambacho kinaitaka Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) baada ya kushauriana na vyama vyote vya siasa na Serikali, kuandaa na kuchapisha katika Gazeti la Serikali Kanuni za Maadili ya Uchaguzi zitakazoainisha maadili ya vyama vya siasa, Serikali na Tume wakati wa kampeni za uchaguzi na uchaguzi na utaratibu wa utekelezaji wake.

Kifungu hicho kinaelekeza kanuni za maadili zitasainiwa na kila chama cha siasa, kila mgombea kabla hajawasilisha fomu ya uteuzi, Serikali na Tume na zitapaswa kuzingatiwa na wahusika wote waliosaini.

Akizungumza kwenye mahojiano maalumu na vyombo vya habari mkoani Dodoma jana Aprili 11, 2025 Mkurugenzi wa Uchaguzi wa INEC, Ramadhani Kailima amesema chama cha siasa ambacho hakitasaini kanuni za maadili hakitaruhusiwa kushiriki kwenye uchaguzi huo.

Kailima amesema tayari maandalizi yote muhimu na mawasiliano yameshafanyika baina ya Tume, Serikali na vyama vya siasa na kwamba, kinachosubiriwa ni kuwasili kwa wahusika jijini Dodoma kwa ajili ya kusaini kanuni hizo za maadili.

Amesema kazi hiyo itafanyika kwa siku moja tu na baada ya hapo chama ambacho hakijasaini kanuni hizo za maadili hakitapata fursa ya kusimamisha wagombea.

Katika mahojiano na kituo cha luninga cha Azam, Kailima amesema mgombea yeyote katika uchaguzi, sheria inamtaka ajaze fomu namba 10 kuthibitisha atazingatia kanuni za maadili.

“Kama chama cha mgombea hakijasaini kanuni za maadili maana yake mgombea hatapata fomu namba 10, hivyo chama husika kitapata haki ya kutosimamisha wagombea kwa sababu kutokusimamisha wagombea ni haki pia siyo lazima,” amesema.

Chadema njiapanda

Wakati akieleza hayo, ndani ya Chadema hakujapatikana mwafaka iwapo Katibu Mkuu wa chama hicho, John Mnyika, kesho ataungana na vyama vingine kwenda jijini Dodoma kusaini kanuni hizo, kama walivyoalikwa na INEC tangu Aprili 4, mwaka huu.

Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Bara), Aman Golugwa amesema uamuzi wa ama kwenda kusaini au kutokwenda umeachwa kwa Mnyika, ambaye pia amesema hayuko tayari kulizungumzia hilo kwa sasa.

Kigugumizi cha Chadema kwenda au kutokwenda kusaini kanuni hizo, kinahusishwa na msimamo wake uliounda ajenda ya No reforms, no election.

Katika hatua nyingine, baadhi ya makatibu wakuu wa vyama vingine vya siasa wameshawasili Dodoma kwa ajili ya kusaini kanuni hizo, huku wengine wakisema wapo njiani kwenda jijini humo.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Golugwa amesema utaratibu unamtaka Katibu Mkuu (Mnyika), kwenda kusaini, hivyo kwa suala hilo linapaswa kuachwa hadi siku husika Aprili 12, 2025.

“Utaratibu unamuhitaji Katibu Mkuu impase kwenda na kusaini zile kanuni, kwa hiyo katika hatua ya sasa tuliache mpaka kesho tuone litakuwaje,” amesema.

Mnyika alipotafutwa na Mwananchi amesema atafutwe siku nyingine kuzungumzia hilo, lakini kwa sasa vema kujielekeza kwenye kile kilichozungumzwa na Golugwa katika mkutano na wanahabari.

“Naomba focus (jielekeze) kwenye kilichozungumzwa katika mkutano wa Naibu Katibu Mkuu, hayo mengine nitafute siku nyingine tutayaongea,” amesema.

Mtazamo vyama vingine

Alipotafutwa na Mwananchi, Mwenyekiti wa Chama cha Ada Tadea, Juma Ali Khatibu amesema kila chama kilipewa taarifa ya kuwasilisha mapendekezo yake kuhusu kanuni za maadili ya uchaguzi.

Baada ya hatua hiyo, amesema siku tano zilizopita INEC imewaandikia makatibu wakuu wa vyama vyote vya siasa kuwaalika jijini Dodoma kwa ajili ya kikao cha kusaini kanuni hizo na tayari katibu mkuu wa chama hicho ameshakwenda kwa ajili ya hilo.

“Kabla ya kusaini zitapitiwa kama kila chama kilivyopendekeza, kisha zitasainiwa. Walioitwa ni makatibu wakuu na hivi ninavyokwambia baadhi tayari wapo njiani kwenda Dodoma hata wa chama changu ameshakwenda,” amesema.

Katibu Mkuu wa Chama cha DP, Abdul Mluya amesema tayari yupo njiani kwenda jijini Dodoma kusaini kanuni hizo.

“Mimi nipo njiani nakwenda Dodoma, sisi tunashiriki kikao tulichoalikwa na tunakwenda kusaini. Mimi kwa kuwa ndiye Katibu Mkuu, nipo njiani kwenda,” amesema.

Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Husna Abdallah amesema chama hicho kitashiriki kikao hicho.

Amesema tayari alishaanza safari ya kwenda Dodoma kuhudhuria mkutano kama alivyopokea mwaliko wa INEC.

“Sisi tunashiriki maana tumealikwa, tulipeleka mapendekezo yetu na sasa ni kwenda kusaini. Hivi tunavyoongea nipo njiani kwenda Dodoma,” amesema.

Kwa upande wa ACT-Wazalendo, Katibu Mkuu wake, Ado Shaibu ameahidi kushiriki.

Amesema kabla ya kikao hicho waliwasilisha mapendekezo 10 kwa INEC kama walivyotakiwa kufanya.

“Tunashiriki bila shaka nami ndiye nitakayekwenda,” amesema.

Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Amos Makalla, alipotafutwa na Mwananchi jana kuzungumzia mkutano huo simu yake iliita pasipo kupokewa.

Hakuna ukomo

Akizungumzia hilo, mwanasheria Jebra Kambole amesema anavyojua kanuni za maadili ya uchaguzi husainiwa na mgombea au chama kinachoshiriki uchaguzi.

Lakini amesema sheria haikuweka ukomo wa muda wa kusaini kanuni za maadili ya uchaguzi, wakati wowote chama au mgombea atasaini.

“Hakuna ukomo wa kusaini kanuni za maadili. Chama au mgombea atasaini muda wowote,” amesema.

Kwa mujibu wa Kambole, uchaguzi unasimamiwa na Katiba na siyo kanuni, hivyo hakuna uwezekano wa chama au mgombea kukosa haki ya kushiriki mchakato huo kwa sababu za kikanuni.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *