
KATIKA msimu huu wa Ligi Kuu Bara vita ya ufungaji imekuwa kali zaidi kuliko misimu uliopita kwa wachezaji wengi kuibuka na kuonyesha makali – mmoja kati yao akiwa ni Jonathan Sowah wa Singida Black Stars.
Takwimu zinaonyesha mshambuliaji huyo ndiye mwenye ufanisi mkubwa katika kufumania nyavu akiwa amefunga mabao mengi ndani ya muda mfupi ukilinganisha na washambuliaji wote wa ligi.
Sowah amefunga mabao tisa katika mechi 10 alizocheza akitumia dakika 750. Hiyo ina maana kuwa anafunga bao kila baada ya dakika 83 – kikiwa ni kiwango cha juu zaidi kwa msimu huu hadi sasa. Kwa lugha nyingine, kila akicheza mechi ni vigumu kuondoka bila bao kutoka kwake.
Tofauti na washambuliaji wengine waliopo kwenye mbio za kiatu cha dhahabu kama Prince Dube, Clement Mzize wa Yanga, Jean Ahoua na Steven Mukwala wa Simba, Sowah alijiunga na Singida Black Stars katika dirisha dogo la usajili msimu huu. Maana yak ni kwamba hakupata nafasi ya kuanza msimu pamoja na wengine, lakini kwa muda mfupi alioupata amefanya kile ambacho wengine wamehangaika kwa miezi kadhaa kukitimiza.
Wakati Dube wa Yanga akiwa kinara wa mabao kwa sasa akifikisha 12 sawa na Ahoua katika dakika 1,595 kwenye mechi 23, anahitaji wastani wa dakika 133 kufunga bao moja. Hata hivyo, Dube kwa sasa ndiye mchezaji aliyehusika na mabao mengi zaidi – 20 ikiwamo asisti nane, huku Clement Mzize akiwa na mabao 11 katika dakika 1,504 sawa na bao moja kila dakika 136. Ahoua wa Simba akiwa kiungo ana mabao 12 kwa dakika 1,457 kwenye mechi 20 akiwa na uwiano wa bao kila dakika 121.
Kama hiyo haitoshi mshambuliaji wa Simba, Steven Mukwala ana mabao 10 ndani ya dakika 736 ikiwa ni bao kila dakika 73, lakini bado amecheza mechi 20 tofauti na Sowah ambaye ameanza kucheza katikati ya msimu na tayari ana mabao 9 ndani ya mechi 10 tu.
Elvis Rupia, ambaye ni mwenzake katika safu ya ushambuliaji ya Singida BS, ana mabao 10 ndani ya dakika 1,500, akiwa na uwiano wa bao kila dakika 150. Mwingine wa Yanga, kiungo Pacome Zouzoua, ana mabao 9 kwa dakika 1,364, sawa na bao kila dakika 151.
Katika mazingira hayo, ni wazi kuwa Sowah ameingia kwa kishindo katika vita ya wafungaji, huku akiweka presha kubwa kwa wale waliomtangulia. Ni vigumu kuamini kuwa mshambuliaji aliyeanza kucheza katikati ya msimu sasa yuko hatua chache tu kufikia waliocheza mechi zaidi ya 20.
MSIKIE SOWAH
Akizungumzia kasi ya ufungaji, Sowah alisema: “Hii ni kazi yangu na ninafurahia kiwango changu. Naamini naweza kufanya zaidi na kuisaidia timu yangu kumaliza katika nafasi ya tatu au ya pili kwenye msimamo wa ligi.”
Mbali na kuwa hatari langoni, Sowah anaonyesha utulivu, uwezo wa kukaa eneo sahihi na kufunga kwa nafasi ndogo, jambo linalomtofautisha na washambuliaji wachezaji wengine.