Championship vita inaendelea kupamba moto

RAUNDI ya 26 ya Ligi ya Championship, inaendelea tena wikiendi hii ambapo baada ya jana kuchezwa mechi tatu, leo zitapigwa mbili kwenye viwanja mbalimbali kwa kila timu kutafuta pointi tatu muhimu, huku ikihitimishwa mingine kesho.

Vinara wa ligi hiyo Mtibwa Sugar yenye pointi 60, huku ikiwa na kumbukumbu ya kushinda mabao 3-1, dhidi ya TMA, mechi ya mwisho kwenye Uwanja wa Manungu Complex, itasalia uwanjani hapo kuikaribisha Mbuni FC iliyoichapa African Sports 4-0.

Mbuni inayotoka jijini Arusha, ina kibarua kigumu kwa wapinzani wake, kwani tangu msimu umeanza, Mtibwa Sugar haijawahi kupoteza au kutoka sare mchezo wowote iliocheza kwenye uwanja wake huo wa nyumbani, jambo linalosubiriwa kitakachotokea.

Mtibwa iliyoshuka daraja msimu uliopita, imecheza mechi 13, kwenye Uwanja wa Manungu Complex kati ya 25 na kushinda zote, huku safu ya ushambuliaji ya kikosi hicho ikifunga jumla ya mabao 34 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara tano.

Mchezo mwingine wa leo, utapigwa kwenye Uwanja wa Mabatini mkoani Pwani ambako maafande wa Green Warriors waliochapwa na Polisi Tanzania mabao 3-2, watacheza dhidi ya Geita Gold, iliyotoka kuichapa Cosmopolitan mechi ya mwisho kwa mabao 4-0.

Raundi ya 26, itahitimishwa kesho Jumapili kwa michezo miwili kupigwa, ambapo Polisi Tanzania iliyoichapa Green Warriors mabao 3-2, itakuwa kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa Babati kucheza na Cosmopolitan, iliyopoteza mbele ya Geita Gold 4-0.

Mchezo wa mwisho, utahitimishwa kwenye Uwanja wa Kituo cha Ufundi cha TFF Kigamboni, ambapo Transit Camp iliyochapwa na Mbeya Kwanza mechi ya mwisho kwa mabao 4-1, itaikaribisha Bigman FC, yenye kumbukumbu ya kutoka suluhu na Kiluvya United.

Kocha Mkuu wa Mbeya Kwanza, Maka Mwalwisi alisema kwa mechi zilizobakia hakuna timu yenye uhakika wa moja kwa moja wa kupanda Ligi Kuu Bara, kushuka daraja au kusalia hivyo, ugumu huongezeka zaidi kutokana na mahitaji ya kila mmoja wao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *