
Dar es Salaam. Vita vya kibiashara kati ya Marekani na China vinaendelea kushika kasi, huku mataifa hayo mawili makubwa kiuchumi duniani yakizidi kutunishiana misuli kwa kupandishiana ushuru, hali inayoibua wasiwasi mkubwa katika masoko ya kimataifa.
Marekani, chini ya uongozi wa Rais Donald Trump, imeongeza ushuru kwa bidhaa za China hadi kufikia asilimia 145. Hii ni baada ya kuanza na ushuru wa asilimia 125, kisha kuongeza asilimia 20 zaidi.
Trump alieleza kuwa hatua hiyo inatokana na “ukosefu wa heshima” wa China kwa masoko ya dunia.
Kwa upande wake, China haijakaa kimya. Tarehe Aprili 11, ilijibu kwa kuongeza ushuru kwa bidhaa za Marekani kutoka asilimia 84 hadi asilimia 125.
Waziri wa Mambo ya Nje wa China, Lin Jian, alisema, “Ikiwa Marekani itaendelea na tabia yake ya ushuru, China itapambana hadi mwisho.”
Mbali na kuongeza ushuru, China imechukua hatua kali zaidi dhidi ya Marekani, ikiweka vikwazo kwa kampuni 18 za Marekani zinazohusika na sekta ya ulinzi, na pia kudhibiti mauzo ya madini adimu kama samarium na gadolinium, ambayo ni muhimu kwa sekta za teknolojia na ulinzi za Marekani.
Katika hatua ya kutuliza mvutano na mataifa mengine, Marekani imetangaza kusimamisha ushuru wa ziada kwa nchi zote isipokuwa China kwa kipindi cha siku 90.
Trump amesema ametoa muda huo kwa nchi ambazo hazikujibu hatua zake za ushuru, akiongeza kuwa, “Niliwaambia kuwa wakijibu, tutapandisha ushuru maradufu.”
Hatua hiyo inalenga kutoa nafasi kwa mazungumzo ya kibiashara na nchi kama Umoja wa Ulaya, Vietnam na Korea Kusini.
Zaidi ya nchi 75 tayari zimewasiliana na Marekani kuanza mazungumzo kuhusu mikataba ya kibiashara, ambapo Vietnam imekubali kuanza rasmi majadiliano ya kurekebisha ushuru wake wa sasa wa asilimia 46.
Athari za mvutano huu tayari zimeanza kuonekana katika masoko ya dunia. Siku ya Alhamisi, Soko la Hisa la Marekani la S&P 500 lilianguka kwa asilimia 3.5 kutokana na hofu ya kupungua kwa biashara kati ya Marekani na China kufuatia ushuru mkubwa wa pande zote mbili.
Kampuni ya tathmini ya biashara ya JPMorgan imetabiri kuwa kuna uwezekano wa asilimia 60 wa uchumi wa dunia kuingia katika mdororo wa kiuchumi, hali ambayo inachochewa na mvutano huu unaoendelea kati ya mataifa hayo mawili.
Wakati dunia ikisubiri kwa tahadhari matokeo ya mazungumzo yanayotarajiwa, mvutano huu wa kibiashara unaendelea kutikisa uhusiano wa kibiashara wa kimataifa, huku athari zake zikiwa mbali zaidi ya Washington na Beijing.