
Dar es Salaam. Wananchi wamesisitizwa wanapokuwa na miradi ya ujenzi kuwatumia wahandisi wabobezi na waliosajiliwa ili kuepuka athari mbalimbali zinazoweza kujitokeza kutokana na ujenzi kufanyika kwa chini ya kiwango.
Wito huo umetolewa leo Aprili 11, 2025 jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Wahandisi Tanzania (IET) katika kongamano lilikowakutanisha wahandisi kutoka kada mbalimbali pamoja na wahandisi tarajali kujadili masuala yanayohusu fani hiyo.
Moses amesema baadhi ya watu kutokana na kutokuwa na uelewa wa kutosha au kutaka kupunguza gharama wamekuwa wakiwatumia mafundi vishoka ambao kimsingi siyo wahandisi.
“Kufanya hivyo ni hatari kwani kumtumia mtu asiye na taaluma ya uhandisi anaweza kutoa ushauri usio sahihi ambao unaweza kusababisha madhara,” amesema.
“Usimchukue mtu kwa sababu amejitambulisha tu kuwa yeye ni mhandisi, jiridhishe kwa kuomba kitambulisho au kufika katika taasisi ili kuhakikisha kama amesajiliwa,” amesema.
Ameshauri ni vyema mtu anapohitaji mhandisi kuonana na taasisi zinazosimamia wanataaluma hao kwani kabla hawajasajiliwa huko huwa ni lazima taasisi ijiridhishe kama amekidhi vigezo.
Vilevile alitumia fursa hiyo kuwakumbusha wahandisi kutimiza wajibu wao kwa kusimamia ujenzi wa miradi kikamilifu.
“Nidhamu, umakini, ufanisi, uwezo, juhudi, weledi, uwajibikaji ni muhimu ili kukidhi matakwa ya maendeleo ya teknolojia na kuweza kusaidia nchi kutatua changamoto katika sekta mbalimbali za kiuchumi, pia kutoa suluhisho la matatizo katika jamii,” amesema.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (Pura), Charles Sangweni amewataka wahandisi kutochukulia teknolojia kama tishio la ajira zao bali wanatakiwa kuongeza ubunifu ili kuendana na kasi mabadiliko ya Sayansi na Teknolojia.
Sangweni amesisitiza umuhimu wa matumizi ya teknolojia katika uhandisi ili kuwa na miradi imara na yenye kudumu kwa muda mrefu.
“Msiichukulie teknolojia kama inakuja kuua ajira zenu, mnapaswa kutafakari kwa kina kuja na ubunifu ambao utaitumia hiyo teknolojia kufanya kazi kwa ufanisi zaidi,” anasema.
Mkuu wa Idara ya Uhandisi wa Kemikali kutoka Chuo Kikuu cha Dar es salaam (UDSM), Mahir Said amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya vyuo vikuu, waajiri pamoja na viwanda katika kuzalisha wahitimu wanaoendana na soko la ajira la sasa.
Pia ametoa wito kwa wahandisi tarajali kuweka fikra zao katika kujiajiri baada ya kuhitimu.
Janeth Kibela ambaye ni mwananafunzi wa fani ya Uhandisi wa kemikali kutoka UDSM ambaye alishiriki katika kongamano anasema uwepo wa makongamano kama hayo ni muhimu kwani unawasaidia wao kama wahandisi tarajali kujua kwa kina yaliyomo katika fani hiyo ikijumuisha changamoto pamoja na fursa.