Dodoma. Serikali imeweka msimamo kuwa mikopo ya asilimia 10 katika kundi la vijana itatolewa kwa watu wenye umri wa mwisho wa miaka 45 pekee.
Hata hivyo, umri huo ni nyongeza ya miaka 10 kutoka kikomo cha awali cha miaka 35, lakini kundi la wanawake halikuwa na ukomo.
Kauli hiyo imetolewa bungeni leo, Ijumaa Aprili 11, 2025 na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Tamisemi, Dk Festo Dugange wakati akijibu swali la Mbunge wa Igalula, Venant Protas.
Katika swali lake, mbunge huyo alihoji kama Serikali haioni haja ya kuongeza umri kwa vijana wa kiume wanaopata mikopo ya halmashauri hadi kufikia miaka 50.

Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tamisemi, Dk Festo Dugange akizungumza wakati akijibu maswali ya wabunge, bungeni leo Ijumaa Aprili 11, 2025 Jijini Dodoma. Picha na Hamis Mniha
Mbunge mwingine aliyeuliza kuhusu ongezeko la wanufaika kufikia umri zaidi ya miaka 50 alikuwa ni Stella Manyanya, aliyesema kundi la wanaume limekuwa halinufaiki kama ilivyo kwa makundi mengine.
Naibu Waziri alisema mikopo ya asilimia 10 inatolewa kwa mujibu wa Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa, Sura ya 290, Kifungu cha 37A cha mwaka 2018, pamoja na kanuni za usimamizi na utoaji wa mikopo kwa Wanawake, vijana na watu wenye ulemavu za mwaka 2024.
Amesema kwa mujibu wa sheria hiyo, mikopo hiyo isiyo na riba hutolewa kwa makundi maalumu ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
“Makundi haya yana fursa ndogo ya kupata mikopo katika taasisi nyingine za fedha kutokana na ukosefu wa dhamana na uwezo mdogo wa kumudu riba. Aidha, umri wa ukomo katika mikopo kwa vijana umeongezwa kutoka miaka 35 hadi 45,” amesema Dk Dugange.
Hata hivyo, amesema Serikali itaendelea kusimamia utoaji wa mikopo hiyo kwa mujibu wa sheria na kanuni zilizopo, na kufanya maboresho pale itakapohitajika ili kuhakikisha ufanisi na uwiano katika utoaji wa fursa hizo.