Unguja. Wadau wameeleza umuhimu wa Tanzania kuridhia Itifaki ya Afrika ya Watu wenye Ulemavu (ADP) ikielezwa ina shabaha ya kulinda, kukuza haki na kutoa fursa za elimu, afya na uchumi bila kubaguliwa.
Moja ya jambo la msingi lililo kwenye mkataba huo lakini halipo katika mikataba mingine ya haki za binadamu ni kukataza kuwanyanyasa au kuwaua watu wenye ualbino kwa imani za kishirikina.
Wamebainisha hayo katika kikao kazi kilichokutanisha vyama vya watu wenye ulemavu na wadau wengine kutoka Zanzibar na Tanzania Bara ikiwa ni sehemu ya kukusanya maoni na kuyawasilisha katika Baraza la Mawaziri ili yapitiwe na kupelekwa kujadiliwa bungeni.
Akizungumza katika kikao hicho leo Aprili 11, 2025 mjini Unguja, Mwenyekiti wa kikundi kazi cha ufuatiliaji wa uridhiwaji wa ADP, Gideon Mandes amesema itifaki hiyo ni ya kipekee kwa sababu ni sheria mahususi inayozingatia haki, heshima na utu wao kuhakikisha mipango yote ya maendeleo katika nchi husika inajumuisha masuala ya walemavu.
Pia inataka wasibaguliwe katika fursa za elimu, afya, ajira na miundombinu.
“Kuna changamoto ambazo tunakumbana nazo za kimila, desturi ambazo zinakwaza haki zetu kwa hiyo mkataba huu umeeleza hayo yote yakiwamo mauaji ya watu wenye ualbino. Nchi ikiridhia itifaki hii, itakuwa inashirikiana na zingine za Afrika kukomesha hali hiyo lakini kubwa zaidi umeeleza wazi wapewe fursa sawa za kiuchumi, siasa na uongozi,” amesema

Mwenyekiti Shirikisho la Vyama vya Watu wenye Ulemavu, Idara ya Wanawake, Nassiria Nasir Ally (wa kwanza kulia) akizungumza katika kikao kazi kuhusu Tanzania kuridhia Itifaki ya Afrika ya Watu wenye Ulemavu (ADP) leo Ijumaa Aprili 11, 2025 Mjini Unguja, Zanzibar.
Mkurugenzi Mtendaji wa shirika linaloshughulikia masuala ya watu wenye ulemavu Tanzania, Mandes amesema itifaki hiyo itasaidia nchi kuangalia sera na sheria zilizopo ama kuzibadilisha au kutunga mpya ili kukidhi matakwa kulingana na masharti yaliyomo.
Amesema itifaki hiyo inatoa wajibu kwa nchi mwanachama kuhakikisha inaweka mipango endelevu, inatenga bajeti kwa watu wenye ulemavu, kuwathamini, lakini wao wenyewe kujitete ili kupata fursa za kutosha.
Pia inatoa haki ya wao kuishi katika familia, hawanyanyaswi kutokana na ulemavu wao wapate fursa zote.
“Tunaomba Serikali zote mbili kuhakikisha itifaki hii inapitia michakato yote muhimu haraka iwezekanavyo ili iweze kuridhiwa na kuifanya kuwa sehemu ya mfumo wa sheria wa nchi. Ikiridhiwa sheria, kanuni zibailishwe kukidhi masharti yaliyomo kuhakikisha watu wenye ulemavu hawaachwi nyuma,” amesema.
Itifaki hiyo ina ibara 44, kuanzia ibara ya kwanza hadi 34 ni mahususi kuhusu haki za watu wenye ulemavu na wajibu wao, ushirikiano wa nchi katika kutekeleza masuala ya watu wenye ulemavu na masuala muhimu ya kiutawala.
Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, Tanzania kuna watu wenye ulemavu milioni 5.2.
Ofisa miradi wa asasi ya kimataifa ya Sightsavers, Magdalena Focus amesema itifaki hiyo ni sehemu ya kuhakikisha mambo ya watu wenye ulemavu yanapewa kipaumbele.
“Tunaomba Serikali iridhie kabla ya Bunge halijamalizika, itakuwa hatua kubwa kwa wananchi wenye ulemavu,” amesema.
Katibu wa Mtendaji wa Baraza la Taifa la Watu wenye Ulemavu Zanzibar, Ussi Khamis Debe amesema maoni haya ni sehemu ya vipengele vitakavyofanikisha kuridhiwa itifaki hiyo.
“Kwa hiyo tunapaswa kuwa na andiko la pamoja kutoka Zanzibar la kuwasilisha serikalini,” amesema.
Ali Omar Makame kutoka Shirikisho la Jumuiya za Watu Wenye ulamavu Zanzibar, amesema wamepokea mchakato huo wakiamini utasaidia Tanzania kusukuma maendeleo ya wenye ulemavu.