
Kwa miaka ya hivi karibuni lugha ya Kiswahili inazidi kuenea na kupaa katika mataifa mengi duniani, kikipata wazungumzaji wapya na hii ni kutokana na juhudi za wakuu wa nchi zinazozungumza lugha hiyo kuitangaza kimataifa.
Kwa mujibu wa takwimu za hivi karibuni, zaidi ya watu milioni 200 wanazungumza lugha ya Kiswahili duniani kwa sasa, na idadi inazidi kuongezeka kila siku kutokana na kinavyotangazwa.
Mbali ya idadi ya watu wengi wanaotoka Zanzibar na Tanzania Bara, pia ipo idadi kutoka Kenya, Uganda, Burundi na nchi za maziwa makuu, ikiwemo nchi ya Kongo DRC wanazungumza Kiswahili kama wanavyokuwa nyumbani kwao.
Baada ya Mapinduzi ya Zanzibar mwaka 1964, Wazanzibari wengi walikimbilia hapa Oman na si ajabu kuona hata Waarabu wazawa wakizungumza kiswahili tena kwa ufasaha kama wanavyozungumza watu wa huko Afrika Mashariki.
Ipo baadhi ya mitaa iliyopachikwa majina kutokana na wingi wa idadi ya watu wanaozungumza Kiswahili, ukiwemo wa Chicago uliopo Amraat katikati ya jiji la Muscat, kwa maana wapo waswahili wengi wanaozungumza Kiswahili.
Wakati wa safari yangu sikuona ajabu Shirika la Ndege la Oman likitoa matangazo yake kwa lugha ya Kiswahili kuwajulisha abiria wake wakati ikijiandaa kutua katika uwanja wa ndege wa Muscat Oman na kuamini kuwa lugha hiyo ina wazungumzaji wengi.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Samia Suluhu Hassan amekuwa akipongezwa kwa kukitangaza Kiswahili kimataifa na mara nyingi amekuwa akihutubia kwa Kiswahili katika majukwaa ya mikutano ya kimataifa.
Juni 13 mwaka 2022, Rais Samia Suluhu Hassan alifanya ziara ya siku tatu hapa Oman, pamoja na mambo mengine wakati akizungumza na Watanzania waishio Oman aliwasihi kudumisha utamaduni wao, licha ya kuwa utamaduni wa Oman na Tanzania unashabihiana na kusema mtu ni kwao.
Katika matembezi yangu mbali ya Oman, pia nimeweza kutembea nchi ya Dubai, Qatar na Bahreen ambako kote Kiswahili kinazungumzwa na hii ni kutokana na idadi ya watu wengi kutoka nchi za Afrika Mashariki wanaofanya kazi na wengine wakiwa ni wazawa wanajifundisha lugha hiyo tamu.
Ukiwa katika moja ya mataifa nchi ya Falme za Kiarabu usijaribu kumteta mtu kwa kudhani hajui Kiswahili na mwisho wake unaweza kuumbuka, kwani lugha hiyo imesambaa katika mataifa hayo na wengi wasiojua kuizungumza hupenda kujifunza.
Katika mataifa haya ya Falme za Kiarabu hakuna nchi hata moja inayofundisha somo la Kiswahili shuleni wala vyuoni, lakini imekuwa maarufu sana baada ya Kiarabu na Kiingereza na huenda kutokana na kuenea lugha hiyo ikaanza kufundishwa.
Nchi ya Misri ambayo iko kaskazini mwa Bara la Afrika, kuna mwamko mkubwa kwa raia wake, hasa wanafunzi wanaosoma vyuo mbalimbali nchini humo wanajifunza Kiswahili ambapo kwa sasa ni ya pili baada ya Kiarabu.
Misri lugha yao ya Taifa ni Kiarabu, lakini kutokana na Kiswahili kuzidi kuenea katika mataifa mbalimbali ya Afrika, Asia, Ulaya na Amerika, hapa Oman pia inaweza kuwa lugha ya pili kuzungumzwa kutokana na watu wengi kutamani kujifunza lugha hiyo.
Kiswahili kimetawala hapa Oman na mgeni akiwa ndani ya uwanja wa ndege hawezi kushangaa kukisikia kinazungumzwa, wakiwemo wafanyakazi na madereva taksi nje ya uwanja ilhali sio wa kutoka mataifa yanayozungumza Kiswahili.
Ndiyo nikasema kwa namna lugha hii inavyopasua anga kimataifa, hapa Oman Kiswahili kinaweza kufundishwa shuleni na vyuoni, hasa ikiwa baadhi ya maneno ya Kiswahili yanashabihiana na lugha ya Kiarabu.
Mwamko wa kuenea Kiswahili hapa Oman unaongezeka kwa kasi kutokana na uhusiano mzuri kati ya Oman na Tanzania na kasi ya raia wa nchi mbili hizi kuamiliana katika mambo mbalimbali, ikiwemo ya kibiashara na kihistoria.
Abudhabi kipo chuo maarufu cha Alqasmia ambacho kina idadi kubwa ya wanafunzi kutoka Afrika Mashariki wanaozungumza kiswahili na kutoa hamasa kwa wenzao kutamani kujifundisha lugha hiyo ambayo kwa sasa inapasua anga kimataifa.
Hapa Muscat kipo Chuo Kikuu ambacho wapo wanafunzi wengi kutoka Afrika Mashariki wanaozungumza Kiswahili na kutoa hamasa kwa wengine kutamani kujifunza lugha hiyo na ndiyo nikasema ukiwa hapa Oman na baadhi ya nchi hizi za Kifalme usithubutu kumteta mtu ukadhani hajui Kiswahili, utaumbuka.
Salim Mohammed ni mwandishi wa habari aliyepo nchi za Falme za Kiarabu.