Sababu Matano kutoonekana Fountain Gate

KUTOONEKANA kwa Kocha Robert Matano kwenye benchi la ufundi la Fountain Gate katika mechi mbili zilizopita za Ligi Kuu Bara, kumeibua maneno mengi zikimuhusisha na kutimuliwa kwake baada ya kutokuwa na matokeo mazuri.

Hata hivyo, uongozi wa klabu hiyo yenye maskani yake mkoani Manyara umesema sababu za kutokuwepo kwa kocha huyo ni kutokana na ajali ya gari aliyoipata hivyo kwa sasa anajiuguza.

Kocha huyo ambaye alitua kikosini hapo Januari 10 mwaka huu kuchukua nafasi ya Mohamed Muya, amekosekana kwenye mechi mbili dhidi ya Mashujaa walipofungwa 3-0 na sare ya 1-1 dhidi ya Pamba Jiji.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mtendaji Mkuu wa Fountain Gate FC, Thabita Kidawawa alisema: “Hakuna taarifa za kumalizana na Matano kutokana na mfululizo wa matokeo mabaya, taarifa ambayo wengi hawafahamu ni kwamba Matano ni mgojwa, alipata ajari ya gari tukiwa Mbeya, dereva akiwa katika harakati za kugeuza gari bila kujua kuna kocha nyuma alimgonga na kumuumiza.

“Hivyo kocha yupo anajiuguza na akirejea katika hali yake ya kawaida atarudi kwenye majukumu yake, suala la kumfukuza halipo na hatutarajii kulifanya kwa hivi karibuni kwani bado tunaamini ana uwezo wa kuiongoza timu yetu na ikafanya vizuri.”

Wakati Matano akikosekana, kikosi hicho kwa sasa kinaongozwa na Kocha Msaidizi Amri Said.

Matano tangu ateuliwe Januari 10, mwaka huu, amekiongoza kikosi hicho katika michezo tisa ya Ligi Kuu Bara, akishinda miwili, sare miwili huku akichapwa mitano.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *