Mapinduzi yaliyoshindwa DRC: Wafungwa 3 warejeshwa Marekani kwa ajili ya kufunguliwa mashtaka

Raia watatu wa Marekani waliohukumiwa kifo nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwa kuhusika katika mapinduzi yaliyofeli ya Mei 19 wamerejea Marekani. Hukumu yao ilibadilishwa na kuwa kifungo cha maisha, na kuondoka kwao kulipangwa kwa ushirikiano na Ubalozi wa Marekani huko Kinshasa. Lakini safari yao ya kisheria bado haijakamilika: sasa watalazimika kujibu mashitaka yanayowakabli mbele ya mahakama ya Marekani.

Imechapishwa:

Dakika 1

Matangazo ya kibiashara

Na mwandishi wetu mjini Kinshasa, Paulina Zidi

Malalamiko yamewasilishwa nchini Marekani dhidi ya Marcel Malanga, Tyler Thompson na Benjamin Zalman. Wanashutumiwa kwa kuanzisha mapinduzi dhidi ya serikali ya kigeni, katika kesi hii ya DRC.

Hati hiyo ya mahakama yenye kurasa 82 inakusanya ushahidi uliokusanywa na ofisi ya FBI ya Salt Lake City, ikisaidiwa na zile za New York na Nairobi. Inarejelea madai ya maandalizi ya operesheni hiyo katika ardhi ya Marekani: ununuzi wa vifaa, mafunzo, pamoja na ratiba yao mjini Kinshasa katika siku zilizotangulia shambulio hilo, hasa kutembelea makao makuu ya Bunge,ni jambo linalozingatiwa kama misheni ya upelelezi. Ripoti hiyo pia inaelezea mlolongo sahihi wa matukio ya Mei 19.

Kulingana na wachunguzi wa FBI, kundi hilo lilitaka kupindua serikali na kumweka Christian Malanga kuwa mkuu wa nchi iitwayo “New Zaire.” Christian Malanga, babake Marcel, aliuawa wakati vikosi vya usalama viliingilia kati mnamo Mei 19.

Mtuhumiwa wa nne wa Marekani

Jina jipya linaonekana katika kesi hii: Joseph Peter Moesser. Huyu ni Mmarekani wa nne aliyehusika katika mapinduzi hayo, ambaye alikamatwa hivi karibuni nchini Marekani. Ingawa hakuwepo mjini Kinshasa, anaelezwa kuwa mtaalamu wa vifaa vya kulipuka wa kundi hilo. Kulingana na uchunguzi huo, watu hao wanne wanadaiwa kujaribu kubadilisha ndege zisizo na rubani za raia kuwa ndege zisizo na rubani za kulipuka kama sehemu ya mpango wao.

Wamarekani watatu waliorejeshwa kutoka DRC wanatarajiwa kufikishwa kwa mara ya kwanza katika mahakama ya Brooklyn, New York, kabla ya kuhamishiwa Salt Lake City. Kuhusu Joseph Moesser, amefikishwamoja kwa moja katika mahakama ya shirikisho huko Salt Lake City Alhamisi, Aprili 10.

Wanaume hao wanne wanakabiliwa na kifungo cha maisha jela kwa tuhuma zinazowakabili.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *