Zimbabwe : Walioandamana kupinga uongozi wa Mnangagwa wanyimwa dhamana

Mahakama nchini Zimbabwe imewanyima dhamana watu karibi 100 waliokamatwa wiki moja iliyopita, wakiandamana kupinga uongozi wa rais Emmerson Mnangagwa.

Imechapishwa:

Dakika 1

Matangazo ya kibiashara

Waandamanaji hao walikamatwa tarehe 31 mwezi Machi, wakishiriki kwenye maandamano katikati ya jiji la Harare, baada ya kuratibiwa na mwanasiasa mkongwe wa chama tawala Blessed Geza, anayetaka rais Mnangagwa kuondoka madarakani, kwa madai kuwa anapanga kuendelea kuwa madarakani hata baada ya kukamilika kwa muhula wake mwaka 2028.

Watu hao wameshtakiwa kwa kusababisha vurugu na kushiriki kwenye maandamano yaliyoharamishwa, makosa ambayo iwapo watapatikana na hatia, watafungwa jela hadi miaka mitano.

Hakimu Isheunesu Matova katika maamuzi yake, amesema amewanyima dhamana kwa sababu za kiusalama na kueleza kuwa, iwapo wataruhusiwa kujumuika na jamii, watasababisha maandamano zaidi.

Maandamano ya mwezi uliopita, hayakuwa makubwa lakini yalisababisha kukwama kwa shughuli za kawaida jijini Harare, huku kukiwa na hofu ya kuzuka kwa vurugu.

Mnangagwa, aliyeingia madarakani mwaka 2017 baada ya mapinduzi ya kijeshi yaliyomwondoa kiongozi wa muda mrefu Robert Mugabe, anashtumiwa  kuwa dikteta anayeongoza kwa mkono wa chuma.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *