
Songea. Jeshi la Polisi Mkoa wa Ruvuma, limesitisha mikutano yote iliyopangwa kufanywa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ukiwamo wa kuhitimisha ziara ya siku sita ya viongozi wakuu wa chama hicho, uliopangwa kufanyika leo.
Leo Alhamisi Aprili 10, 2025 Chadema ilipanga kufanya mkutano wa hadhara katika uwanja wa Matalawe, ikiwa ni sehemu ya kuhitimisha ziara ya siku sita ya viongozi wakuu wakinadi ajenda ya No Reforms No Election katika mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma.
Wakati polisi wakieleza hayo, Makamu Mwenyekiti wa Chadema (Bara), John Heche amekiri kupokea barua kutoka Jeshi la Polisi inayowataka kusitisha mara moja mchakato wa mkutano wao wa hadhara uliopaswa kuhutubiwa na Mwenyekiti wao, Tundu Lissu anayeshikiliwa na polisi jijini Dar es Salaam.
“Kama mnavyoona tulifuata taratibu zote za maandalizi, lakini hapa kuna barua ya polisi ya zuio, ila huu ni ushahidi wa ukiukwaji wa haki za binadamu, tutaupeleka unakotakiwa.”
“Nawashukuru mliojitokeza kuja kutusikiliza hii ni nchi ya kwetu sote, kwa vile wameleta barua hii tunakwenda kushauriana na viongozi namna ya kuliendea jambo hilo. Nawaahidi tutarudi tena Songea,” amesema Heche akizungumza na wananchi wa Matalawe.
Awali, akizungumza na wanahabari Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Marco Chilya alisema Jeshi hilo limesitisha rasmi kibali cha kufanya mkutano wa hadhara wa Chadema na wameshazungumza na viongozi wa chama hicho akiwamo Heche.
Kamanda Chilya amewataka wananchi wote na viongozi kutofanya mikutano na kutawanyika kuendelea na shuguli zao za kila siku na watakao kaidi, watachukuliwa hatua za kisheria.
Athibitisha polisi kumshikilia Lissu
Katika hatua nyingine, Kamanda Chilya amethibitisha kumshikilia Lissu aliyekamatwa jana Jumatano Aprili 9 wilayani Mbinga, akisema kwa sasa anahojiwa jeshi hilo jijini Dar es Salaam.
Amewataka viongozi wa vyama vya siasa kutotoa matamko au lugha zozote za uchochezi.
“Natoa onyo kwa vyama vyote vya siasa, kutotoa maneno ya uchochezi au lugha ya kukashifu polisi au serikali katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu wa 2025,”
“Yeyote atakayebainika kufanya vitendo hivyo, atachukuliwa hatua kali za kisheria,”amesema Kamanda Chilya.