ACT-Wazalendo yahofia kupuuzwa mageuzi sheria za uchaguzi, wagusia suala la Lissu

Dar es Salaam. Chama cha ACT-Wazalendo kimeonyesha wasiwasi kuhusu kutoweka kwa matumaini ya kupatikana kwa mabadiliko na utekelezaji wa sheria za uchaguzi, kuelekea Uchaguzi Mkuu wa baadaye Oktoba 2025.

Kutoweka kwa matumaini hayo, kunatokana na kile kilichoelezwa na chama hicho kuwa, hotuba ya bajeti ya ofisi ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliyoitoa bungeni jana Jumatano, iliyotarajiwa kutoa mwafaka kuhusu hilo, haukugusia kabisa.

Pamoja na hali hiyo, Makamu Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo Bara, Issihaka Mchinjita amesema wataendelea na mapambano ya demokrasia na mabadiliko ya sheria na kanuni za uchaguzi.

Sambamba na hilo, amegusia hatua ya kukamatwa kwa Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu alipokuwa ziarani mkoani Ruvuma, akisema ni ishara kwamba Serikali imepoteza dhana ya uvumilivu na ustahimilivu.

Mchinjita ameyasema hayo jijini Dar es Salaam leo, Alhamisi Aprili 10, 2025, alipochambua hotuba ya bajeti ya ofisi ya Waziri Mkuu, Majaliwa aliyoitoa bungeni Dodoma jana.

Kukosekana mwafaka kuhusu mabadiliko ya sheria za uchaguzi ndani ya hotuba hiyo, amesema kunaonyesha Serikali haina nia ya kufanya chochote kuhusu hayo.

“Ni dhahiri kuwa Serikali haina mpango wa mabadiliko yoyote kuelekea uchaguzi mkuu 2025,” amesema Machinjita.

Ameeleza kupitia hotuba hiyo, Serikali ilitarajiwa kutoa uelekeo utakaoleta mwafaka wa kitaifa kuhusu mabadiliko ya sheria na mifumo ya uchaguzi.

“Lakini hotuba imegeuka kuwa mwiba mkali kwa wadau wa uchaguzi, kwani hakuna mwelekeo wowote wa mabadiliko wala utekelezaji wa sheria za uchaguzi,” amesema.

Kilichomsikitisha, amesema ndani ya hotuba hiyo, Majaliwa amesema demokrasia nchini imeimarika ilhali kuna changamoto lukuki.

“Kauli hiyo ni ya Serikali kiziwi isiyosikiliza na kujali maoni ya wananchi,” amesema.

Hata hivyo, amegusia mambo wanayotamani yafanyiwe mabadiliko ambayo ni Makamishna wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) wapatikane kwa ushindani, wakurugenzi wa halmashauri wasiwe wasimamizi wa uchaguzi wa majimbo.

Pia, amesema mawakala wa vyama vya siasa wafanye kazi zao bila bughudha, wagombea wasienguliwe, pasiwe na kura feki na vyombo vya ulinzi na usalama visiingilie mchakato wa uchaguzi.

Kukamatwa kwa Lissu

Katika hatua nyingine, Mchinjita ameeleza kitendo cha kukamatwa kwa Lissu ni mwendelezo wa kukosa ustahamilivu wa dola na Serikali, pia ni shambulio la wazi kwa demokrasia na vyama vya upinzani.

“Natumia nafasi hii kulitaka Jeshi la Polisi kumwachia mara moja bila masharti yoyote Mwenyekiti wa Chadema ili aendelee na shughuli zake za kisiasa kama walivyopanga,” amesema.

Ameeleza imeshuhudiwa viongozi wa CCM wakifanya ziara bila bughudha, na kwa kuwa huu ni mwaka wa uchaguzi, vyama vyote viachwe vifanye kazi kwa usawa.

Kwa ujumla, amesema hotuba hiyo ikitarajiwa ingejibu changamoto za wananchi, lakini imejaa hadaa na kile alichokiita ujanjaujanja.

Kuhusu suala la ajira, amesema Serikali inapaswa kutengeneza mazingira yatakayotoa fursa za kuajiri wananchi wengi, ikiwemo kutekeleza miradi.

Ameitaka Serikali kuwekeza vya kutosha kwenye sekta ya kilimo kwa kuhakikisha upatikanaji wa uhakika wa mbolea, viwanda vidogovidogo na vikubwa vya kuongeza thamani ya mazao.

“Tunaitaka Serikali itekeleze miradi mikubwa kama kiwanda cha gesi asilia (LNG) cha Lindi itakayozalisha mamilioni ya ajira kwa vijana kuanzia uzalishaji wa gesi, usambazaji na matumizi.

“Pia, mradi wa chuma na makaa ya mawe wa Mchuchuma na Liganga. Kuharakishwa kwa ujenzi wa miradi hii kutasaidia kuzalisha ajira nyingi nchini,” amesema.

Jambo lingine alilopendekeza ni Serikali itoe ajira za kutosha kwa waalimu, watumishi wa afya na wataalamu wengine kulingana na mahitaji ili kupunguza uhitaji uliopo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *