
Morogoro. Kesi inayowakabili watu 14 wanaotuhumiwa kwa kujifanya maofisa wanaotoa ajira, wakiwakusanya vijana 48 kutoka sehemu mbalimbali nchini na kujipatia fedha kinyume na sheria, imeahirishwa hadi Aprili 24, 2025 itakapotajwa tena.
Kesi hiyo inasikilizwa katika Mahakama ya Mwanzo mjini Morogoro (Nunge) ambapo katika hati ya mashtaka, watuhumiwa hao wanashtakiwa kwa kujifanya maofisa wenye mamlaka ya kutoa ajira kinyume na kifungu cha sheria 369 (1) cha kanuni ya adhabu sura 16 K/A 2023.
Watuhumiwa hao walishitakiwa Aprili Mosi, 2025 saa 9 alasiri huko Azimio Kilolo, Kihonda Wilaya ya Morogoro kwa kujifanya maofisa wenye mamlaka ya kutoa ajira na kuwakusanya vijana 48 kutoka sehemu tofauti nchini na kujipatia fedha huku wakijua ni kosa kisheria.
Hakimu Mkazi Mahakama ya Mwanzo Mjini Morogoro (Nunge), Beatha Richard ameeleza kuwa ameahirisha kesi hiyo hadi Aprili 24, 2025 kutokana na upande wa mlalamikaji ambaye ni Mkuu wa Operesheni wa Wilaya ya Morogoro, Geoffrey Kalugendo kupata dharura.
Kabla ya kuahirishwa kwa kesi hiyo, Hakimu Beatha ameeleza kuwa washtakiwa wote dhamana zao bado zinaendelea, hivyo watakuwa nje baada ya kukana kutenda makosa hayo.
Katika mashtaka hayo ya jinai namba 174/2025, wanaotuhumiwa ni pamoja na Kenedy Mwanza, Maghembe Nyorobi, Mashaka Jajiro, Lasoy Lazier, Sahenga Sokala, Hajard Habibu, Zaina Habibu, Elenuru Moleli, Ericky Francis, Baraka Ally, Daud Joshua, Anitha Elirehema, Donard Edward na Dickson Akyoo.
Akitoa maelezo ya udhuru mahakamani hapo, Koplo Mohamed Musaa amemueleza Hakimu Mkazi, Beatha Riachard kuwa Mkuu wa Operesheni wa Wilaya ya Morogoro amepata majukumu mengine ya ujio wa Mwenge wa Uhuru ambao utazindua na kufungua miradi mbalimbali ya maendeleo mkoani Morogoro.
Mwenge wa uhuru 2025 utapokewa katika Wilaya ya Morogoro, tarafa ya Ngerengere, katika uwanja wa Kijiji cha Mgude, kesho Aprili 11, 2025 ukitoka Mkoa wa Pwani ambako ulizinduliwa kitaifa ukibeba kaulimbiu: “Wananchi jitokezeni kushiriki uchaguzi mkuu 2025 kwa amani na utulivu”.