Waziri Jafo aipongeza Absa Tanzania kuzindua mkopo mpya wa mali

Dar es Salaam. Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Selemani Jafo amezitaka taasisi za kifedha kuiga mfano wa Benki ya Absa kwa kuja na huduma ya mikopo ya kumiliki mali mbalimbali ikiwemo magari, mashine au vifaa vya kazi bila gharama kubwa.

Huduma hiyo inaitwa Mkopo wa Mali za Kibiashara wa Absa (CAF), na inalenga kurahisisha upatikanaji wa vifaa muhimu kwa biashara mbalimbali nchini, ili waweze kujiendeleza na kufikia malengo yao.

Kupitia mkopo huo, biashara zinaweza kupata hadi asilimia 80 ya thamani ya mali mpya kutoka Ulaya na hadi asilimia 70 kwa mali mpya kutoka China, huku mali hiyo ndiyo itakayokuja kusimama kama dhamana ya mkopo atakaochukua mtu.

Akizungumzia huduma hiyo hivi karibuni wakati wa uzinduzi, Waziri Jafo alisema ni muhimu sana kuwekeza katika mazingira bora ya biashara ili kuwezesha uchumi wa nchi kukua kwa haraka.

Aidha, Waziri Jafo ameongeza kuwa ni jukumu la Serikali kuhakikisha kuwa kuna miundombinu bora, huduma za kibenki na ulinzi wa haki za wamiliki wa biashara.

“Katika kuelekea kwenye uchumi wa kisasa, Serikali inaendelea kuwekeza kwa wajasiriamali na wafanyabiashara kufanikiwa. Hii ni sehemu ya mikakati ya Serikali ya kuongeza ushindani wa biashara na kuhakikisha kuwa nchi inakuwa na mazingira bora ya kufanyia biashara kwa ustawi wa watu wote,” alisema.

Awali, Murugenzi Mtendaji wa Absa Tanzania, Obedi Laiser amesema huduma hiyo imebuniwa kwa ajili ya kusaidia biashara zinazokosa mtaji wa kununua vifaa muhimu.

Hiyo ni kwa sababu wafanyabiashara wataweza kupata wanachohitaji bila kukosa fedha za kuendesha shughuli nyingine.

“Kupitia CAF, biashara zinaweza kukua, kuongeza uzalishaji na kuchangia uchumi bila kuathiri fedha zao za kila siku,” amesema.

Amesema katika mtazamo wa kibiashara CAF ni sehemu ya juhudi za Absa kusaidia biashara kukua na kufanikisha ndoto zao, kwa kauli mbiu yao ya “Kuiwezesha Afrika ya Kesho, Pamoja, Stori Moja Baada ya Nyingine.”

Absa pia inalenga kufanya huduma ya CAF kuwa chaguo la kwanza kwa wafanyabiashara wanaotaka mkopo wa kununua mali. Watatoa masharti mazuri ya kulipa mkopo, faida za kikod, na bima za kulinda mali dhidi ya majanga mbalimbali.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *