
Babati. Jeshi la Polisi Mkoa wa Manyara linamshikilia mwanamke aliyewajeruhi watoto wake wawili kwa kuwachoma na kisu tumboni kwa kile kinachodaiwa kuwa ana msongo wa mawazo.
Mwanamke huyo mwenyeji wa Kata ya Kiomboi, Wilaya ya Iramba mkoani Singida, Prakseda Prosper (29) amewajeruhi watoto wake wawili kwa kisu tumboni akiwa Wilaya ya Babati mkoani Manyara.
Inadaiwa kuwa chanzo cha tukio hilo ni msongo wa mawazo uliosababishwa na kuzaa watoto hao na wanaume tofauti na wao kutopatiwa matumizi ya kila siku.
Akizungumza na vyombo vya habari leo Alhamisi Aprili 10, 2025, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara, Kija Mkoyi amesema tukio hilo limeokea Aprili 2, 2025 katika Mtaa wa Sinai, Kata ya Maisaka wilayani Babati.
Kamanda Mkoyi amesema Polisi walipata taarifa kuwa kuna mwanamke amewajeruhi watoto wake wawili, ndipo walipokwenda eneo la tukio na kumbaini mama huyo amejifungia chumbani kwa shangazi yake akiwa na watoto wake.
Amesema baada ya kumkuta mtuhumiwa amejifungia, Polisi walibomoa chumba na kumkuta na watoto wake wawili, kisu na yeye akiwa amejijeruhi tumboni.
Kamanda huyo amesema mmoja wa watoto hao ana miaka mitano na mwingine ana mwaka mmoja, ambapo mkubwa anasoma darasa la awali.
“Baada ya kumkamata, tulimhoji na kumpeleka Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Manyara akiwa na watoto wake na wanaendelea na matibabu,” amesema Kamanda Mkoyi.
Amesema mwanamke huyo ataendelea kuwa chini ya ulinzi mkali wa Polisi na mara baada ya kupona na uchunguzi ukikamilika atafikishwa mahakamani.
Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Manyara, Dk Michael Haule amethibitisha kupokea watoto wawili na mama yao ambao walijeruhiwa na kitu chenye ncha kali.
Dk Haule ameeleza kwamba tangu wamewapokea wagonjwa hao, siku tano zimepita lakini wanaendelea vizuri.
Amesema mama huyo alikutwa na jeraha kwenye ngozi ya tumbo na mtoto mkubwa jeraha linafanana na majeraha hayajagusa viungo vya ndani kama utumbo na vingine ila mtoto mdogo alikutwa na jeraha lililoenda ndani zaidi na kutoboa utumbo mdogo wa chakula.
Amesema mtoto huyo amefanyiwa upasuaji na kuweka kwenye chumba cha uangalizi maalumu ndani ya siku tano bila kula kitu chochote.
“Jana Aprili 9, alianza kula na mama yake pamoja na mtoto mkubwa walimaliza matibabu lakini bado tuko nao kwa uangalizi zaidi,” amesema Dk Haule.
Dk Haule amesema wanalihusisha tukio hilo na sonona kwa hatua za awali lakini wanaendelea kufanya uchunguzi zaidi.
Amesema ni vizuri mtu akiwa na msongo wa mawazo akaa na ndugu zake hasa anapokuwa na changamoto hiyo ili waweze kumsaidia.
“Tupendane na tushirikishe watu mambo yetu ili watupe ushauri ambao utatusaidia kutoka kwenye msongo wa mawazo,” ameeleza.
Baadhi ya wakazi wa eneo hilo la Sinai, wameeleza kwamba tukio hilo limewasikitisha kwani mwanamke huyo hana ndugu wengine baada ya shangazi yake kusafiri.
Mmoja kati ya wakazi hao, Amina Seleman amesema tukio hilo limewasikitisha na kuwapa hofu mpaka watu wengine wanaogopa kupita eneo hilo.
“Huyu mwanamke amezaa na wanaume wawili tofauti na wote wamemtelekeza, sasa watoto wakilia njaa inakuwa kipengele kwake na hana shughuli za kujipatia kipato,” amesema.