
China siku ya Alhamisi imeshutumu “matamshi ya kutowajibika” ya Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky baada ya kudai kuwa Beijing ilijua kuwa Wachina walikuwa wakiandikishwa na Urusi kuisaidia kupigana nchini Ukraine.
Imechapishwa: Imehaririwa:
Dakika 2
Matangazo ya kibiashara
“Tunashauri pande zinazohusika kuwa na maoni ya haki na ya kuridhisha kuhusu jukumu la China na kutotoa matamshi ya kutowajibika,” Lin Jian, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China amesema siku ya Alhamisi. Alikuwa akijibu swali kuhusu taarifa za Volodymyr Zelensky wakati wa mkutano wa mara kwa mara na waandishi wa habari.
“Serikali ya China siku zote imekuwa ikiwataka raia wake kukaa mbali na maeneo yenye migogoro” na “hasa kuepuka kushiriki katika operesheni za kijeshi za upande wowote,” Lin Jian amebainisha.
Siku ya Jumatano Volodymyr Zelensky alisema kwamba Kyiv ilikuwa na habari juu ya raia 155 wa China wanaoisaidia Moscow katika uvamizi wake. Alidai siku moja kabla, siku ya Jumanne, kwamba jeshi la Ukraine liliwakamata wanajeshi wawili wa China katika jimbo la Donetsk, mashariki mwa Ukraine. Rais wa Ukraine pia alihakikisha kwamba China ilijua kwamba makumi ya raia wake walikuwa wakiajiriwa na Urusi kupigana katika ardhi ya Ukraine.
“Ningependa kusema kwamba China sio sababu ya mgogoro wa Ukraine wala si mshirika wake. “Sisi ni wafuasi wenye nguvu na waendelezaji wa suluhisho la amani,” msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China ameongeza.
Kuhusu mzozo huo, China inataka kuheshimiwa kwa uadilifu wa eneo la nchi zote, ikiwa ni pamoja na Ukraine, na kujionyesha kama nchi isiyoegemea upande wowote ambayo inaweza kusaidia kupata suluhu la kisiasa. Beijing, hata hivyo, haijawahi kulaani hadharani Moscow kwa operesheni yake ya kijeshi na imeimarisha uhusiano wake wa kiuchumi, kijeshi na kisiasa na jirani yake wa Urusi tangu uvamizi huo uanze mnamo mwezi Februari 2022.
Msimamo wa China mara nyingi hukosolewa na nchi za Magharibi, ambazo mara kwa mara huitaka diplomasia ya China kuweka shinikizo kwa Urusi kusitisha vita.
Mamlaka ya Urusi “inachochea nchi nyingine kwenye vita.” “Nadhani sasa wanaiingiza China katika vita hivi,” Volodymyr Zelensky aliliambia kundi la waandishi wa habari, ikiwa ni pamoja na shirika la habari la AFP, Jumatano. Hii ni “hatua ya makusudi kuelekea upanuzi wa vita” na anathibitisha kwamba Moscow inataka “kurefusha mapigano,” alisema.