Video ya wabunge wa Kenya wakipigana yasambaa mtandaoni

Nairobi. Wabunge wawili wanawake wa Bunge la Kenya wamenaswa kwenye video wakipigana nje ya viwanja vya Bunge hilo.

Video hiyo inaonyesha mbunge wa kuteuliwa katika Bunge la Kitaifa, Umi Harun na mwenzake kutoka Bunge la Afrika Mashariki (Eala), Falhada Iman wakivutana hadi kuangushana chini, huku watu wengine wakijaribu kuwatenganisha.

Katika video hiyo iliyorekodiwa na mtu aliyekuwa kwenye viwanja vya Bunge, wabunge hao wawili pia wanasikika wakibishana kwa maneno.

Mmoja afunguka

Umi baadaye alitoa taarifa akieleza tukio hilo kama la kusikitisha, akieleza kuwa amewasilisha malalamiko rasmi.

“Leo, tukio la kusikitisha limetokea katika viwanja vya Bunge hali ambayo naijutia sana kama mbunge na pia kama mama. Mwenzangu kutoka Bunge la Eala ambaye amekuwa na tofauti za muda mrefu na kazi yangu alichukua hatua ambayo siwezi kuikubali,” amesema Umi.

Ameongeza kuwa anajutia tukio hilo na atatoa maelezo zaidi kuhusu suala hilo.

Ingawa huenda Umi akafikishwa mbele ya kamati ya mamlaka na hadhi ya bunge la nchi hiyo kuhusiana na tukio hilo, bado haijafahamika ni hatua gani zitachukuliwa dhidi ya Falhada, ambaye ni mbunge wa Eala anayehudumu Arusha, hivyo huenda asiwajibike chini ya kanuni za Bunge la Kenya.

Bado haijajulikana iwapo Spika wa Bunge la Kitaifa, ambaye ndiye kiongozi wa Bunge, atatoa taarifa rasmi kuhusu tukio hilo au hatua yoyote itakayochukuliwa dhidi ya viongozi hao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *