Orlando, Mamelodi, Al Ahly, Pyramids kitawaka nusu fainali CAFCL

Johannesburg. suluhu waliyoipata Orlando Pirates jana katika mchezo wa pili wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya MC Alger kwenye Uwanja wa Orlando nchini Afrika Kusini, iliipeleka timu hiyo nusu fainali kwa faida ya bao moja walilopata kwenye mchezo wa kwanza uliochezwa ugenini.

Orlando imefuzu hatua ya nusu fainali kwa ushindi wa jumla wa bao 1-0 ambalo lilifungwa na Mohau Nkota katika mechi ya kwanza iliyochezwa Aprili Mosi mwaka huu kwenye Dimba la Ali La Pointe, Algeria.

Timu hiyo imeungana na Mamelodi Sundowns zote za Afrika Kusini zitakazocheza hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo dhidi ya timu za Misri. Mamelodi itakutana na mabingwa watetezi Al Ahly huku Orlando Pirates ikicheza na Pyramids FC.

Michezo ya nusu fainali ya kwanza itachezwa kati ya Aprili 18 na 19, 2025 kisha marudiano ni kati ya Aprili 25 na 26 ambapo Orlando Pirates itaanzia nyumbani kukabiliana na Pyramids kwenye Uwanja wa Orlando huku Mamelodi nao wakiwa nyumbani Uwanja wa Loftus Versfeld, Pretorial kuvaana na Al Ahly.

Itashuhudiwa kwa mara ya pili katika nusu fainali ya mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika timu mbili kutoka taifa moja kucheza na zingine mbili za taifa lingine tangu ilipotokea mwaka 2020 zilipokutana Wydad ya Morocco dhidi ya Al Ahly ya Misri na Raja Casablanca (Morocco) dhidi ya Zamalek (Misri).

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *