Unguja. Chama cha ACT-Wazalendo kime wataka baadhi ya viongozi kuacha tabia ya kuwagombanisha Wazanzibar na kusababisha kuuana kwa kisingizio cha Uchaguzi.
Kimewataka viongozi hao kuacha mara moja kutekeleza nia zao ovu kupitia mwamvuli huo.
Hayo yamesemwa leo Alhamis Aprili 10, 2025 na Mwenyekiti wa chama hicho Taifa, Othman Masoud Othman alipofanya mazungumzo na viongozi wa ACT Wazalendo huko Mtambile, Mkoa wa Kusini Pemba.
Othman ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, amesema wananchi wa Zanzibar wamechoshwa na machafuko ya makusudi yanayowakabili katika kila msimu wa uchaguzi tangu kuanzishwa kwa mfumo wa siasa wa vyama vingi.
“Wazanzibari tunasema tumechoka kuuliwa kwa sababu za uchaguzi na fitna za kisiasa, tumechoka kugombanishwa kwa kisingizio cha uchaguzi, itoshe kwa baadhi ya watawala kutekeleza nia zao ovu, kwa kupitia ‘mwavuli’ huo,” amesema Othman na kuongeza;
“Kwa nini maafa na mashambulizi yanaelekezwa zaidi kwa wananchi wa Unguja na Pemba? Je Tanzania bara kakuna wapinzani na ushindani wa siasa wa vyama vingi,” amehoji.
Mbali na hayo, Othman amewahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi kupigania na kutekeleza haki yao ya kidemokrasia na wazingatie kukataa unyonge wa kudhulumiwa ili kufanikilisha lengo la msingi la kuiokoa Zanzibar.
Naye, Makamu Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo Zanzibar, Ismail Jussa amesema harakati za ukombozi wa nchi, zilikuja zikiwahusisha watu wote kwa ajili ya maslahi mapana ya Taifa na sio kwa kuwanufaisha watu binafsi.

“Tumeona wazee wetu waliopigania haki zetu, walipata matatizo yakiwamo kufukuzwa kazi, kunyanyaswa na hata baadhi yao kuuawa, lakini hawakuvunjika moyo, waliendelea kupambana, dhamira yao haikuwa kupigania vyeo bali ilikuwa kuipigania Zanzibar,” amesema Jussa.
Ametoa wito kwa wanachama wa chama hicho kutumia haki yao ya kidemokrasia bila malumbano na nongwa.
“Hakuna mwenye hati miliki ya jimbo, kila mwanachama anayo haki ya kugombea ila kwa maslahi mapana ya wananchi na nchi kwa ujumla,” amesema Jussa.
Kikao hiki ni mwendelezo wa ziara ya mwenyekiti huyo kukutana na viongozi wa ngazi zote za Chama hicho katika mikoa mitano ya Zanzibar.