Kesi ya mauaji ya bilionea wa madini na mwanaye yapigwa kalenda

Songea. Kesi ya mauaji ya kukusudia ya mfanyabiashara tajiri wa madini, Marwa Masese Senso na mwanaye, imeahirishwa hadi Aprili 23, 2025 baada ya wakili wa Serikali anayeendesha kesi hiyo, Generosa Montana kupata changamoto.

Kesi hiyo imekuwa ikivuta hisia za wadau wa haki jinai na wananchi wengine kutokana na namna vifo hivyo vilivyotokea ikidhaniwa walifariki dunia kwa ajali ya gari lakini baada ya uchunguzi, polisi walidai kubaini  yalikuwa mauaji ya kukusudia.

Kulingana na hati ya mashitaka, katika shitaka la kwanza, washtakiwa wanadaiwa kuwa Agosti 29, 2023 katika eneo lisilofahamika kati ya Mbeya na Songea katika barabara kuu ya Mbeya-Songea, walimuua John Marwa Masese.

Katika shitaka la pili, inadaiwa Agosti 29, 2023 huko kijiji cha Lilondo katika wilaya ya Songea Mkoa wa Ruvuma, washtakiwa walimuua Marwa Masese Senso. Marehemu wote ni wakazi wa Kunduchi Jijini Dar es Salaam.

Kesi hiyo ya mauaji, ilikuwa iendelee jana Aprili 9, 2025 kwa ajili ya usikilizwaji wa hatua za mwanzo za kuhamisha kesi kutoka Mahakama ya Hakimu Mkazi Songea kwenda Mahakama Kuu ya Tanzania.

Hata hivyo, kesi hiyo ilipoitwa mbele ya Hakimu Mkazi, Michael Manjale, wakili huyo wa Serikali alisema  amepata changamoto (bila kuitaja), hivyo kuomba mahakama kuahirisha kesi hiyo.

Akijibu hoja hiyo, kiongozi wa jopo la mawakili wa utetezi, Peter Madeleka alipinga vikali ombi hilo kwa kusema kwamba limelenga kuchelewesha haki za wateja wao bila sababu za msingi kisheria, akinukuu Ibara ya 107A(2)(a) ya Katiba ya Tanzania.

Wakili Madeleka aliiomba Mahakama kutochelewesha haki bila sababu za msingi, lakini hata hivyo baada ya kusikiliza pande zote mbili, Hakimu aliahirisha kesi hiyo hadi Aprili 23, 2025 itakapokuja kwa ajili ya kutajwa, licha ya upelelezi kukamilika.

Ibara hiyo ndogo ya Katiba inasema katika kutoa uamuzi wa mashauri ya madai na jinai kwa kuzingatia sheria, Mahakama itafuata kanuni ya kutenda haki kwa wote bila kujali hali ya mtu kijamii au kiuchumi bila sababu ya msingi.

Uahirishwaji wa usomaji wa ‘Committal’ wa jana unafanya shauri hilo liwe limeahirishwa kwa mara ya sita katika hatua hiyo kutokana na sababu mbalimbali.

Tayari Mahakama Kuu imezuia kutajwa majina ya mashahidi na maeneo wanapoishi baada ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) kuwasilisha maombi ya jinai ya mwaka 2025 na Jaji Emmanuel Kawishe kuyaridhia Aprili 3,2025.

Maombi hayo ambayo yalisikilizwa upande mmoja (Ex-Parte) bila washtakiwa kuwepo, yalikuwa dhidi ya wajibu maombi ambao ni Kadari, Erasto Swai, Joseph Komba, Alfred Milinga, Grace Senso, Sarah Bundala na Elizabeth Ndunguru.

Hoja kuzuia majina

Wakati wa usikilizwaji wa maombi hayo, DPP aliwakilishwa na Wakili Mwandamizi wa Serikali, Generosa Montano na Wakili wa Serikali, James Robby ambao walisisitiza mashahidi na washtakiwa ni ndugu na wengine ni wa damu.

Generosa alimweleza Jaji kuwa mshtakiwa wa pili, Erasto Swai, Joseph Komba (wa tatu) na Elizabeth Ndunguru (wa saba) ni ndugu wa mama mmoja, wakati mshtakiwa wa kwanza, Kadari ni mume wa mshtakiwa wa sita, Sarah Bundala.

Wakili huyo wa Serikali alimweleza Jaji kuwa mshtakiwa wa tano, Grace Senso ni mama mzazi wa mshtakiwa wa sita na mmoja wa marehemu katika hati ya mashitaka, Marwa Senso ni kaka wa mshtakiwa wa tano.

Marehemu John Masese, anayedaiwa kuuawa na washtakiwa ilielezwa alikuwa mwajiriwa wa mama mzazi wa mshtakiwa wa kwanza, hivyo kutolewa maelezo ya kutowatambulisha mashahidi na kuwaweka katika hatari.

Wakili alisema hadi maombi hayo yanasikilizwa, mmoja wa mashahidi muhimu wa Jamhuri ambaye hata hivyo hakumtaja, amekufa kifo cha ajabu na kwa mazingira hayo aliomba majina ya mashahidi wote yalindwe na yasitajwe.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *