
Wanaume watano wanaoshutumiwa kuwa katika makundi yaliyopigwa marufuku ya Kiislamu kutka dhehebu la Kisunni wamenyongwa nchini Iran, kulingana na mashirika yasiyo ya kiserikali, yakiwataja kama “wafungwa wa kisiasa” waliohukumiwa kifo baada ya kesi isiyo ya haki.
Imechapishwa:
Dakika 1
Matangazo ya kibiashara
Wanaume hao watano wamenyongwa Jumatano, Aprili 9, katika gereza la Vakilabad huko Mashhad, jiji lililo mashariki mwa nchi hiyo, bila familia zao kufahamishwa mapema au kupewa fursa ya kuwatembelea mara ya mwisho, shirika la Iran la Human Rights (IHR) lenye makao yake makuu Norway limesema katika taarifa yake.
“Wafungwa hawa waliteswa na kuhukumiwa kifo baada ya kesi isiyo ya haki,” amesema mkurugenzi wa IHR Mahmood Amiry-Moghaddam, ambaye amewataja watu hao watano kama “wafungwa wa kisiasa.”
Mashtaka ya “uasi”
Wanne kati yao walikuwa wa jamii ya Waislamu kutoka madhehebu ya Sunni nchini Iran, kundi la walio wachache katika Jamhuri ya Kiislamu yenye Washia wengi. Wa mwisho kunyongwa alikuwa Mshia. Wote walikamatwa mwaka wa 2015 katika kesi ya muongo mmoja na kukutwa na hatia ya “baghi,” shtaka la “uasi” chini ya sheria ya Kiislamu ya Iran, kutokana na uanachama wao katika makundi yaliyopigwa marufuku ya Kiislamu kutoka madhehebu ya Kisunni. Washtakiwa wenzao watatu katika kesi hiyopia walinyongwa mnamo Desemba 2020.
“Wanaume wengine watano wameuawa… baada ya kesi za uwongo ambazo hazikuwa na ukweli wowote wa uhalali au haki,” amesema Behnam Daraeizadeh, mtafiti katika Kituo cha Haki za Kibinadamu cha New York nchini Iran (CHRI). Shirika la Habari la Wanaharakati wa Haki za Kibinadamu lenye makao yake nchini Marekani (HRANA) limeripoti kwamba familia zilifahamu tu kuhusu mauaji hayo kupitia simu na walikuwa bado wanasubiri nje ya gereza kupokea miili ya wapendwa wao.
Iran, nchi ya pili kwa ukubwa duniani kutekeleza hukumu ya kifo, tayari imewanyonga watu 245 mwaka huu, kulingana na Taasisi ya Kimataifa ya Sheria ya Kibinadamu (IHR), ambayo ilionya juu ya ongezeko la kutisha la idadi ya watu walionyongwa.