
SINGIDA Black Stars, leo huenda ikasogea hadi nafasi ya tatu katika msimamo wa Ligi Kuu Bara na kuishusha Azam FC, ikiwa itashinda dhidi ya Coastal Union, huku wapinzani wake wakipoteza au kutoka sare mbele ya Yanga.
Iko hivi. Singida Black Stars inayoshuka kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga na Coastal Union kuanzia saa 10:00 jioni endapo itashinda itafikisha pointi 53 kutoka 50, kabla ya Azam yenye pointi 51 kuikabili Yanga saa 1:00 usiku.
Singida Black Stars imecheza michezo 25, ambapo inashika nafasi ya tatu na pointi 51, ikishinda 15, sare sita na kupoteza minne.
Hivyo, ushindi utaipeleka hadi nafasi ya tatu, huku ikisubiri kitakachojiri kati ya Azam na Yanga usiku, wakati kwa Coastal Union iko nafasi ya 13 na pointi 25 baada ya kushinda mechi tano, sare 10 na kupoteza 10.
Singida Black Stars inaingia mchezoni baada ya kuichapa nyumbani Azam FC bao 1-0, Aprili 6, huku Coastal Union ikitoka kuchapwa ugenini 1-0 na ya Yanga, Aprili 7. Coastal inayorejea kwenye Uwanja wa Mkwakwani ikicheza mara ya kwanza msimu huu baada ya dimba hilo kufanyiwa marekebisho, inakabiliwa na matokeo mabovu ikiwa imecheza michezo minane ya ligi mfululizo bila ya kuonja ladha ya ushindi.
Katika michezo hiyo imetoka sare minne na kuchapwa pia minne, huku mara ya mwisho kushinda ilikuwa 2-1 dhidi ya JKT Tanzania, Februari 7, mwaka huu, ikikabiliwa pia na safu butu eneo la ushambuliaji.
Katika michezo minane imefunga bao moja na kuruhusu manane, sawa na wastani wa kuruhusu bao moja kila mchezo, jambo illilosababisha kuondolewa Kocha Juma Mwambusi.
Mwambusi aliyejiunga na kikosi hicho Oktoba 23, 2024, akichukua nafasi ya Mkenya David Ouma aliondoka Aprili 6, 2025, baada ya kuiongoza katika michezo 16, ya Ligi Kuu kati ya hiyo alishinda mitatu, sare minane na kupoteza mitano, timu ikifunga mabao 11 na kuruhusu 16, huku Mwambusi akiiacha ikiwa nafasi ya 12 na pointi 25.
Mchezo ambao ulikuwa wa kichapo cha bao 1-0 dhidi ya Yanga, Aprili 7, alisimamia Kocha Joseph Lazaro, hivyo anakabiliwa na kibarua kingine cha kupambania ushindi wa kwanza tangu arithi mikoba ya Mwambusi.
Kwa upande wa Singida, inaingia ikiwa haijapoteza mechi tano mfululizo zilizopita baada ya kushinda minne na sare moja, huku mara ya mwisho kupoteza ilikuwa mabao 2-1 dhidi Yanga, Februari 7, 2025.
Kocha wa Coastal Union, Joseph Lazaro alisema kitendo cha kurudi katika uwanja wa nyumbani kitarejesha matumaini ya kufanya vizuri kutokana na sapoti kubwa ya mashabiki, huku akiwaomba kuendelea kuwaunga mkono.
Kocha wa Singida, David Ouma alisema licha ya kutambua ugumu wa mchezo, lakini wamejipanga kiakili na kimwili ili kuendelea kuishi katika malengo ya kupigania nafasi nne za juu.
JKT TZ VS NAMUNGO
Huo ni mchezo wa saa 8:00 mchana utakaopigwa kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Mbweni jijini Dar ambapo timu hiyo ya maafande iliyopo nafasi ya sita na pointi 31 itapambana dhidi ya Namungo inayoshika nafasi ya 11 na pointi 27.
JKT ina kumbukumbu ya kulazimishwa sare ya mabao 2-2 na Dodoma Jiji – mchezo wa mwisho uliopigwa Uwanja wa Isamuhyo Aprili 3, huku Namungo FC ikiwa na morali baada ya kuichapa KMC 2-1, Aprili 6.
Katika michezo mitano iliyopita ya ligi baina ya timu hizo, JKT imeshinda miwili na sare mitatu, huku mara ya mwisho Namungo kushinda ilikuwa ni wa bao 1-0 nyumbani Julai 4, 2020.
Kocha wa JKT Tanzania, Ahmad Ally alisema makosa ya kinidhamu katika eneo la kujilinda yaliyowagharimu mchezo uliopita wameyafanyia kazi, huku Juma Mgunda wa Namungo akiwataka wachezaji kuwaheshimu wapinzani wao.
MASHUJAA FC VS TABORA UNITED
Mchezo mwingine utakaopigwa saa 10:00 jioni utakuwa kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika mjini Kigoma ambapo Mashujaa FC iliyopo nafasi ya tisa na pointi 27 itapambana dhidi ya Tabora United inayoshika nafasi ya tano na pointi 37.
Mchezo huo utakuwa kipimo kingine kwa Kocha Mkuu wa Tabora United Mzimbabwe Genesis ‘Kaka’ Mangombe ambaye tangu ajiunge na kikosi Machi 28, 2025 akichukua nafasi ya Mkongomani Anicet Kiazayidi hajashinda mechi.
Tangu ateuliwe katika michezo mitatu amepoteza yote akianza wa hatua ya 16 bora ya Kombe la Shirikisho (FA) akichapwa na Kagera Sugar kwa penalti 5-4, baada ya sare ya 1-1.
Baada ya hapo, Mangombe akaiongoza timu hiyo katika michezo miwili ya ligi na yote akachapwa akianza na 3-0 nyumbani dhidi ya Yanga, Aprili 2, kisha ugenini 1-0 dhidi ya Pamba Jiji, Aprili 5.
Hata hivyo, mchezo huu utakuwa ni wa kisasi kwa Mashujaa FC kwa sababu mechi ya kwanza walipokutana kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora, Tabora United ilishinda bao 1-0 lililofungwa na Morice Chukwu kwa penalti, Novemba 4, 2024.
Mbali na kisasi hicho, tangu Tabora United ipande Ligi Luu 2022-2023 haijapoteza mchezo wa michuano hiyo dhidi ya Mashujaa, kwani mara tatu zilipokutana imeshinda mbili na moja sare ya 1-1, Desemba 5, 2023.
Akizungumzia mchezo huo, Kocha wa Mashujaa FC, Salum Mayanga alisema ushindi wa mwisho wa mabao 3-0 dhidi ya Fountain Gate umeamsha morali ya wachezaji kutokana na kutokuwa na mwenendo mzuri, ingawa changamoto imekuwa eneo la kujilinda.
Kocha wa Tabora United, Mangombe alisema licha ya presha kubwa kutokana na mwenendo wa kikosi hicho, lakini taratibu anaendelea kuingiza falsafa zake kikosini.