Kibaha. Upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama si changamoto tena kwa wananchi takriban 6,000 wa vijiji vya Kwala na Mwembengozi wilayani Kibaha, Mkoa wa Pwani, baada ya kukamilika kwa mradi wa maji uliogharimu Sh1 bilioni.
Kabla ya mradi huo, wananchi hao walilazimika kutembea umbali mrefu kutoka vilipo vijiji hivyo kwenda vijiji vya jirani kufuata huduma ya maji safi na salama.
Taarifa ya kukoma kwa changamoto hiyo, imetolewa leo, Jumatano Aprili 9, 2025 na Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (Ruwasa) Wilaya ya Kibaha mkoani Pwani, Debora Kanyika, alipozungumza mbele ya kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa, Ismail Ussi.

“Ujenzi wa mradi huu ulianza mwaka 2023 na mpaka sasa umekamilika na utahudumia wananchi wa vijiji vya Kwala na Mwembengozi ndani ya Wilaya ya Kibaha,” amesema.
Amesema katika utoaji wa huduma ya maji kwa wananchi watazingatia kanuni na taratibu zilizopo ili kuhakikisha mradi huo unakuwa na manufaa kwa wengi.
Mkazi wa Kijiji cha Kwala, Khadija Hussein, amesema kukamilika kwa mradi huo kutaondoa changamoto zilizokuwa zinawakabili ikiwemo homa za matumbo kwa kutumia maji yasiyo salama.
Kwa upande wa Joseph Mwanyika anayeishi Kwala, amesema ukosefu wa huduma ya maji ulihatarisha ndoa zao, kwa kuwa wanawake walikuwa wakiamka usiku kufuata huduma hiyo visimani.

Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakari Kunenge, amesema upatikanaji wa maji katika mkoa huo kwa sasa umeimarika kutokana na kukamilika miradi mbalimbali.
“Tunajua huduma ya maji ni muhimu kwa wananchi hivyo tumeendelea kujenga miradi katika maeneo mengi ndani ya mkoa wetu,” amesema.
Ussi amewataka watendaji wa Ruwasa kuutunza mradi huo ili utoe huduma kwa wananchi kwa miaka mingi.
“Nawaomba watendaji wa Ruwasa utunzeni mradi huu na mtoe huduma kwa kuzingatia taratibu zilizopo,” amesema.
Mwenge huo, umezindua miradi 13 ya maendeleo yenye thamani ya Sh10 bilioni.