Kauli ya RPC Geita kuhusu ukamataji yawaibua wadau wa haki jinai

Geita. Kauli ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Saphia Jongo, inayowaasa wananchi kutokubali kukamatwa na polisi wasiojitambulisha, imeibua mijadala miongoni mwa wadau wa haki jinai nchini, wakitaka kauli hiyo ifanyiwe kazi katika mikoa yote ili kukabiliana na wimbi la utekaji.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Aprili 8, 2025, baada ya kutoa mafunzo ya polisi jamii na ulinzi shirikishi kwa watendaji wa kata, vijiji, wenyeviti na maofisa tarafa, Kamanda Jongo aliwataka wananchi kutokubali kukamatwa na mtu yeyote anayedai kuwa askari polisi bila kuonyesha kitambulisho halali na kueleza kituo cha polisi alikotoka.

Kamanda Jongo alisisitiza kuwa kitendo cha polisi kumkamata raia bila kujitambulisha na kutoa kitambulisho halali, ni kinyume cha sheria na huenda ikawa mbinu ya kuficha vitendo vya kihalifu.

Alisema kumekuwa na matukio ya utekaji yanayodaiwa kufanywa na watu waliovaa sare za polisi na kutumia magari yanayodaiwa kuwa ya Serikali, lakini bila kutoa uthibitisho wowote kwa wananchi, jambo linalotia hofu na kuathiri imani ya wananchi kwa vyombo vya dola.

“Askari wa kweli anapokwenda kukamata mtu, lazima ajitambulishe kwa jina, awe na kitambulisho cha kazi na aseme anatoka kituo gani. Ikiwa hana hivyo, huyo si askari ni mtu wa kawaida anayeweza huenda akawa jambazi au mhalifu,” alisema Kamanda Jongo.

Alisema kuwa sheria inamtaka polisi anayefanya upekuzi kwa mtu kuwa na mtu mzima wa kushuhudia, ingawa si lazima mtu huyo awe mwenyekiti wala mtendaji wa kijiji.

Kauli hiyo inakwenda sambamba na mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai iliyoundwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwamba kuna umuhimu wa kupunguzwa kwa taasisi za ukamataji na kuhifadhi wahalifu ili kuondoa malalamiko ya wananchi kuhusiana na ukamatwaji wa ndugu zao.

Tume hiyo ilipendekeza kazi ya ukamataji ibakie kuwa ya Jeshi la Polisi ili iwe rahisi kwa ndugu wa watuhumiwa kujua mahali alipohifadhiwa ndugu yao, lakini pia mahabusu za polisi ndizo pekee zitumike kuhifadhi watuhumiwa wa makosa ya jinai.

Pia, Kanuni za Kudumu za Jeshi la Polisi (Police General Orders) au kwa kifupi PGO, zinatoa mwongozo wa ukamataji, ikiwamo mtuhumiwa kufahamu tuhuma zake.

Wadau wa haki jinai wapongeza

Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Onesmo Ole Ngurumwa, akizungumza na Mwananchi leo Jumatano, Aprili 9, 2025 amempongeza Kamanda Jongo kwa uthubutu na kusema kauli hiyo ni ya mamlaka, itakayowafanya askari wa ngazi ya chini kuwa makini.

Amesema pia kauli hiyo itazuia watu wanaotaka kufanya uhalifu kwa kujifanya askari washindwe kufanya uhalifu kwa kuwa tayari wananchi wamepata elimu na kutiwa nguvu na kamanda wa polisi.

“Utaratibu wa kwenda kukamata unamtaka askari awe na sare, gari la jeshi na ajitambulishe. Pia wanaokuja kukamata wanapaswa kuwa na kiongozi wa eneo hilo. Wakishajitambulisha wanapaswa wamruhusu mhusika kuwasiliana na ndugu zake na waeleze kituo cha polisi wanachompeleka,” amesema Ole Ngurumwa.

Amesema kauli iliyotolewa na RPC Geita inapaswa kuigwa na viongozi wote wa mikoa na wawasisitize askari wao wa chini wazingatie sheria ya ukamataji, hasa kipindi hiki chenye wimbi la utekaji.

“Katika wimbi hili la utekaji, lazima watu wajiridhishe kama hawa ni polisi, kama polisi watafuata sheria, watajitofautisha na watekaji,” amesema.

Aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Hellen Kijo-Bisimba amesema kwa mujibu wa sheria, polisi anapokwenda kukamata kwa njia ya kawaida anapaswa kujitambulisha na kumueleza mhusika sababu za kumkamata.

Amesema licha ya sheria kueleza wazi, lakini mara nyingi kinachofanyika ni kama utekaji na si ukamataji, kutokana na askari wanaofanya hivyo kutofuata sheria.

“Polisi lazima ajitambulishe na amwambie mtu kosa lake. Hata kama ni tukio la kushtukiza mtu amefanya hapohapo, anamuweka chini ya ulinzi, anajitambulisha na kumueleza kosa, ndipo amchukue,” amesema Bisimba.

Wakili Peter Madeleka amesema kitendo kilichofanywa na RPC Jongo ni cha kijasiri na amekuwa mkweli kwa wananchi.

Amesema kwa mujibu wa sheria ya ukamataji, kifungu cha 14(1) kinaeleza namna ukamataji unavyopaswa kufanywa, na inaeleza askari anapotaka kumkamata mtuhumiwa anapaswa kuwa na hati ya ukamataji na kufuata utaratibu wote kwa kujitambulisha na kumwambia mtuhumiwa kosa lake.

“Mimi kama Wakili wa Mahakama Kuu ya Tanzania naungana na kauli ya Kamanda wa Polisi Geita kwa sababu ni inaendana na sheria. Askari anayefanya ukamataji bila kujitambulisha anakuwa si askari, bali ni mtekaji na mhalifu kama wahalifu wengine, na mwananchi ana haki ya kujilinda katika mazingira kama hayo,” amesema Madeleka.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *