
Dar es Salaam. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewasilisha bungeni mapitio ya utekelezaji wa shughuli za Serikali na mwelekeo wa mwaka ujao wa fedha, akitilia mkazo mambo manne, ukiwemo uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu.
Masuala mengine aliyoyazungumzia ni kukamilika kwa maandalizi ya Dira ya Taifa, kuimarishwa kwa ukusanyaji wa mapato huku akisisitiza wananchi wajiandikishe kupiga kura pamoja na amani na utulivu katika kipindi cha uchaguzi.
Majaliwa ameyasema hayo leo, Jumatano, Aprili 9, 2025, wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya ofisi yake na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2025/2026, bungeni jijini Dodoma.
Majaliwa amewataka viongozi wa dini, vyama vya siasa na mashirika yasiyo ya kiserikali, kuhamasisha wananchi wazingatie amani na utulivu wakati wa uchaguzi.
Amesema hilo liambatane na kuwahamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi siku ya uchaguzi ili kuwachagua viongozi – Rais, wabunge na madiwani.
Msisitizo huo umekuja huku kukiwa na vuguvu linaloendeshwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) katika maeneo mbalimbali nchini, likilenga kuzuia uchaguzi huo, endapo hakutakuwa na mabadiliko katika mfumo na sheria za uchaguzi.
Hata hivyo, katika hotuba hiyo itakayojadiliwa kwa siku tano hadi Aprili 15, 2025, Majaliwa amesema Serikali imekamilisha marekebisho ya sheria zinazohusu uchaguzi kwa lengo la kuimarisha utawala wa demokrasia.
Amezitaja sheria hiyo kuwa Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani, pamoja na kufanya marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa.
Amesema Serikali tayari imekamilisha utungaji wa kanuni za Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ili kuiwezesha kutekeleza majukumu yake huku yenyewe ikiendelea na maandalizi ya uchaguzi huo kwa kuratibu na kusimamia uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Mpigakura.
Amesema kufikia Machi 2025, awamu ya kwanza ya uboreshaji wa daftari hilo ilikuwa imekamilika Bara na Zanzibar, huku maandalizi ya awamu ya pili yakiendelea.
“Nitumie nafasi hii kutoa rai kwa wananchi wote wenye sifa kujitokeza kuhakiki taarifa zao kabla ya kukamilika kwa awamu ya pili ya uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Mpigakura,” amesema Waziri Mkuu.
Majaliwa ameomba kuidhinishiwa Sh595.29 bilioni, kati ya hizo Sh183.82 bilioni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na Sh411.47 bilioni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.
Fedha hizo ni ongezeko la Sh244.3 bilioni ukilinganisha na Sh350.99 bilioni alizoziomba mwaka 2024/2025
Kadhalika, ameomba kuidhinishiwa Sh186.79 bilioni kwa ajili ya Mfuko wa Bunge, kati ya hizo, Sh174.96 bilioni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na Sh793.33 milioni za maendeleo, sawa na ongezeko la Sh4.98 bilioni ukilinganisha na Sh181.81 bilioni alizoziomba mwaka 2024/2025.
Jambo lingine alilowekea mkazo, ni maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo kwa kuhakikisha wananchi na viongozi wanapata muda wa kutosha kujadili na kutoa maoni na maoni hayo yazingatiwe.
Pia, amewataka maofisa masuuli wa wizara, idara zinazojitegemea, wakala na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) waendelee kuimarisha juhudi za ukusanyaji mapato.
“Wafanye hivi ili kuongeza uwezo wa taifa kujitegemea, pamoja na kubana matumizi katika maeneo yasiyokuwa na tija katika utoaji wa huduma kwa wananchi,” amesisitiza Majaliwa.
Ajira milioni 8
Akizungumzia utekeleza wa ahadi za Serikali, amesema kuanzia Novemba 2020 hadi Februari 2025, ajira milioni 8.08 zimezalishwa kwenye sekta ya umma na binafsi.
Kuzalishwa kwa ajira hizo, amesema kunatokana na Serikali kubuni na kutekeleza mikakati mbalimbali ya kuzalisha fursa kupitia uwekezaji na utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati.
Miongoni mwa miradi hiyo, ametaja ujenzi wa bomba la mafuta ghafi la Afrika Mashariki, reli ya kisasa, Bwawa la Kufua Umeme la Julius Nyerere na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato.
Pia, amesema Serikali imeweka mazingira wezeshi kwa sekta binafsi kukua na kupanua wigo wa uzalishaji wa ajira nchini.
Mapato SGR
Waziri mkuu amesema tangu kuzinduliwa kwa safari za treni ya kisasa Agosti 1, mwaka jana, abiria 1,809,983 wamesafirishwa hadi Februari 2025 na Sh54.9 bilioni zimekusanywa.
“Kuwepo kwa huduma hiyo ya treni, umepunguza muda wa safari kati ya Dar es Salaam na Dodoma kutoka wastani wa saa 10 kwa basi hadi kati ya saa tatu na nne,” amesema.
Vilevile, Majaliwa amesema hadi kufikia Februari, mwaka huu ujenzi wa reli kipande cha kutoka Mwanza – Isaka chenye urefu wa kilomita 341 umefikia asilimia 62.37.
Amesema ujenzi wa kipande cha Makutupora – Tabora chenye urefu wa kilomita 368 umefikia asilimia 14.53, Tabora – Isaka (kilomita 165) asilimia 6.33 na Tabora – Kigoma ( kimomita 506) asilimia 7.34.
Aidha, amesema maandalizi ya kuanza ujenzi wa kipande cha Uvinza – Malagarasi – Musongati ( kilomita 282) yameanza na Serikali za Tanzania na Burundi zimeshasaini mkataba tangu Januari 29, 2025.
Kuhusu mradi wa bomba la mafuta kutoka Uganda hadi Tanga lenye urefu wa kilomita 1,443, Majaliwa amesema umefikia asilimia 55.
Katika mradi huo, amesema Serikali tayari imeshachangia mtaji wa dola za Marekani milioni 376 sawa na asilimia 15 ya hisa na jumla ya ajira 6,610 za muda na 114 za kudumu zimezalishwa.
Waziri mkuu pia amezungumzia kukua kwa uchumi kwa wastani wa asilimia 5.5 mwaka 2024, ikilinganishwa na asilimia 5.1 mwaka 2023.
Ukuaji huo, amesema ulitokana na kuongezeka kwa uzalishaji wa umeme, uimarishaji wa huduma za jamii, kuongezeka kwa mikopo kwa sekta binafsi, kuendelea na ujenzi wa miundombinu ya usafirishaji na kuimarika kwa sekta ya uchukuzi.
“Sekta zilizokuwa na kiwango kikubwa cha ukuaji katika kipindi cha marejeo ni pamoja na shughuli za sanaa na burudani asilimia 17.1, fedha na bima asilimia 16.3 na habari na mawasiliano asilimia 14.3,” amesema.
Kwa upande wa mfumuko wa bei kwa mwaka 2024, amesema umepungua hadi kufikia wastani wa asilimia 3.1 ikilinganishwa na wastani wa asilimia 3.8 mwaka 2023.
Kiwango hicho, amesema kipo ndani ya lengo la nchi na Jumuiya za kikanda la wigo wa asilimia 3.0 hadi 5.0 katika muda wa kati.
Amesema kupungua kwa mfumuko wa bei kulitokana na utekelezaji wa sera madhubuti za fedha na bajeti, kuwepo kwa utoshelevu wa chakula nchini na uboreshaji wa miundombinu ya uchukuzi.
Kuhusu sekta ya ardhi, amesema katika kipindi cha Julai, 2024 hadi Februari, 2025, Programu ya Kupanga, Kupima na Kumilikisha imepima viwanja 7,550 katika mikoa ya Morogoro, Tanga, Kilimanjaro, Dodoma na Njombe.
Kuhusu upangaji wa miji, amesema michoro ya mipangomiji yenye viwanja 126,935 iliidhinishwa na hatimiliki za viwanja 3,569,994 kubadilishwa kuwa za kidijitali.
Tahadhari ya Ukimwi
Maambukizi ya Ukimwi ni jambo lingine alilogusia katika hotuba hiyo, akisema watu 1,536,842 kati ya 1,690,948 wanaoishi na virusi vya ugonjwa huo wanatambua hali zao za maambukizi.
Amesema waathirika 1,545,880 wanatumia dawa za kufubaza makali ya VVU, kati yao watu wazima wenye umri wa miaka 15 na kuendelea ni asilimia 96.4.
Amesema kiwango cha maambukizi mapya ni watu 60,000 kila mwaka, kati yao vijana wakiwa ni takribani asilimia 34.3 ya maambukizi mapya.
“Nitoe rai kwa Watanzania wote kuendelea kuchukua tahadhari kwa kuwa Ukimwi bado ni tishio kama takwimu zinavyoonyesha,” amesema.