
Dar es Salaam. Pamoja na kuwepo upinzani ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kuhusu ajenda ya ‘No reforms, no election,’ ((bila mabadiliko, hakuna uchaguzi) viongozi wa chama hicho, wameendelea kuchanja mbuga katika mikoa mbalimbali kuinadi huku wakiungwa mkono na maelfu ya wananchi.
Viongozi wa chama hicho, wapo katika mikoa ya kusini kwa ziara ya siku sita kutoa elimu kuhusu ajenda ya bila mabadiliko hakuna uchaguzi, inayolenga kushinikiza Serikali kufanya mabadiliko ya mfumo wa uchaguzi na yasipotekelezeka, wameazimia kuzuia uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu.
Katika ziara hiyo iliyotanguliwa na ya awali Kanda ya Nyasa, kumeshuhudiwa umati wa wananchi wakifurika katika mikutano ya hadhara huku wengine wakisimamisha hata misafara ya viongozi.
Ziara hiyo itakayohitimishwa kesho Alhamisi Aprili 10, 2025 wilayani Songea Mkoa wa Ruvuma, inaongozwa viongozi wakuu Tundu Lissu (mwenyekiti) John Heche (makamu mwenyekiti bara) pamoja na wajumbe waandamizi wa kamati kuu akiwamo Godbless Lema.
Pamoja na hoja ya ‘No reforms, no election,’ msisitizo unaotolewa na viongozi hao katika ziara hiyo iliyofanyika mikoa ya Lindi, Ruvuma na Mtwara kwa viongozi wakuu kujigawa makundi mawili ili kuwafikia wananchi kuzuia uchaguzi huo.
Sambamba na hilo, katika ziara hiyo, fumbo la mbinu gani itakayotumika kuzuia uchaguzi huo, limefumbuliwa, baada ya mwenyekiti wa chama hicho, Lissu kuweka wazi kuwa, siku ya uchaguzi wataitisha maandamano.
Ndani ya Chadema, kuna upinzani ‘No reforms no election’ kutoka kundi la G55 la watia nia ubunge wa mwaka 2020 na 2025 likijumuisha baadhi ya vigogo wanaokubaliana kwamba No reforms, si kuzuia uchaguzi wakisema kwa mazingira ya sasa jambo hilo haliwezekani.
Wakati Chadema ikiwa na msimamo wa No reforms, no election, G55 imepinga hatua hiyo jambo ambalo viongozi wakuu wa chama wakiwatafsiri kuwa ni wasaliti na wanaokwenda kinyume na uamuzi wa chama hicho.
Kutokana na upinzani huo, baadhi wenyeviti wa kanda wameanza kuwaandikia barua wakitakiwa kujieleza kwanini wasichukuliwe hatua saini zao kuonekana katika waraka wa G55 wenye hoja tisa za kuitaka Chadema ishiriki uchaguzi huku ukiwa na kichwa cha habari ‘ushauri kwa chama.’
Hata hivyo, G55 wanatafsiri hatua ya kuwataka kujieleza ni kama ubepari ndani ya Chadema na kwamba kuwa na maoni mbadala hakupaswi kuonekana kama wasaliti au uadui.
Kwanini ‘No reforms, no election’
Hii ni moja ya hoja iliyoibuka katika ziara hiyo, ikizungumzwa karibu katika kila mkoa. Viongozi wa Chadema wametaja mambo sita kwanini wamepanga kuuzuia uchaguzi.
Kwa maneno mengine, iwapo mambo hayo yatarekebishwa kabla ya uchaguzi mkuu mwaka huu, chama hicho kitaingia kushiriki uchaguzi huo mara moja.
Akiwa wilayani Namtumbo mkoani Ruvuma katika mwendelezo wa ziara hiyo, Lissu ametaja mambo hayo ni kubadilishwa kwa utaratibu wa mgombea kupita bila kupingwa, mabadiliko ya kuenguliwa kwa wagombea na uandikishaji wa wasio na sifa stahiki.
Mengine ni kuwekwa utaratibu wa kukomesha fujo dhidi ya vyama vya upinzani wakati wa kampeni, uhuru wa mawakala wa vyama vya upinzani na kukomeshwa kwa mauaji wakati wa uchaguzi.
“Hatutaki kufanyiwa fujo tena kwenye kampeni zetu tunazofanya, mawakala wa vyama vyote wawe huru kufanya shughuli zao, ikiwamo kujua kura zao na kama hakuna mawakala, uchaguzi usifanyike, hatutaki kuona uchaguzi unaotoa kafara za watu ili wapate uongozi,” amesema Lissu.
Lissu amesema bila mabadiliko katika mambo hayo, wananchi hawatawapata viongozi sahihi watakaowajibika kuwatetea na kuwasemea.
Maandamano siku ya uchaguzi
Miongoni mwa hoja iliyotikisa katika ziara hiyo ni kauli ya Lissu aliyewahutubia wananchi wa Masasi mkoani Mtwara kuwa, Chadema itaandamana siku ya uchaguzi ili kuzuia mchakato huo.
Lissu amesema watahamasisha wananchi kuandamana endapo Serikali haitafanya mabadiliko ya sheria na kanuni za uchaguzi, akisema hakuna sheria Tanzania inayolazimisha watu kushiriki chaguzi alizoziita za kijinga.
Chaguzi huru na haki
Katika wilaya alizopita Heche katika ziara hiyo, amesisitiza kuwa, Chadema inataka kuwepo kwa uchaguzi huru, haki na unaoaminika ili kupata viongozi bora watakaoendesha Tanzania.
“Changamoto zilizopo ikiwamo namna ya kuongoza Serikali kutetea rasilimali za Taifa, zinaweza kurekibishika na kuzinyoosha zikakaa vizuri, kinachohitajika ni uchaguzi huru na haki, unaoaminika,” amesema Heche.
“Chadema imesema haitakwenda katika uchaguzi wowote bila kuwepo kwa mabadiliko ya sheria. Hatuwezi kupata uchaguzi wa huru na haki katika mazingira tulionayo sasa hivi, pasipo kubadilisha sheria,” amesisitiza Heche.
‘No reforms, no election’ imechelewa
Baadhi ya wachambuzi wa siasa waliozungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti wamesema ‘No reforms, no election’ ni ajenda nzuri, lakini kwa mazingira ya sasa hawaoni kama utekelezaji wake utafanikiwa ni vema Chadema ikajiandaa na mchakato wa uchaguzi.
Mchambuzi Dk Onesmo Kyauke amesema hoja ya ‘No reforms, no election’ imechelewa, akisema kwa chama makini hivi sasa kingeshaanza mchakato wa kumpata mgombea urais na wabunge watakaopeperusha chama chao katika uchaguzi mkuu.
“Kwa chama makini hadi sasa wangeshajua nani na nani watagombea wapi ili wagombea waanze maandalizi ya awali ya uchaguzi, lakini unaposema ‘No reforms, no election’ halafu haipo wazi, kwamba chama kitashiriki au kususia unaleta sitofahamu,”amesema Dk Kyauke.
“No reforms, no election, inawaweka njia panda Chadema, ingawa ziara yao nzuri kwa sababu kila wanaposimama wanazungumzia chaguzi huru na haki, ila mkakati wa bila mabadiliko hakuna uchaguzi umechelewa na hauna manufaa kwa Chadema,” amesema Dk Kyauke.
Amefafanua pale ambako chama kingetakiwa kujikita kusaka fedha za uchaguzi au kuainisha wagombea wanaofaa, lakini chenyewe kinazungumzia ‘No reforms, no election.’
“Kwa mfano hiyo mikutano inayoendelea, wangeitumia kuwaomba uungwaji mkono kwa wagombea wao, lakini hakuna linalofanyika. Wakija kushtuka na kushiriki uchaguzi, muda umeshaisha na wagombea wengine watakimbilia vyama vingine,”amesema Dk Kyauke.
Dk Kyauke ameishauri Chadema kutafakari upya suala hilo, hasa kwa mazingira ya sasa aliyodai utekelezaji wake hauwezi kufanikiwa.
Mchambuzi mwingine wa siasa, Said Msonga amesema unapotafakari kufanya mabadiliko ya sheria lazima uhusishe Bunge lililopewa mamlaka kwa mujibu wa Katiba.
“Unapozungumzia mabadiliko, leo lazima ufikirie Bunge ili lifanye kazi yake ya kikatiba, sasa jana (Jumanne), Bunge la 12 la bajeti lilianza vikao jambo ambalo ndilo la mwisho kabla ya kuvunja. Kwa maana hiyo hakuna nafasi kwa miswada mipya kuletwa,”amesema Msonga.
Amesema kama nafasi haipo, vyama vya upinzani vikiongozwa na Chadema, vinalazimika kusubiri hadi Bunge lijalo ili kuwasilisha hoja za mapendekezo ya mabadiliko wanayoyahitaji ili kujadiliwa.
“Upinzani ukiwamo Chadema wanachotakiwa kufanya kama wanataka mabadiliko ya sheria kwa njia ya kikatiba wanapaswa kujiandaa kuwania nafasi za ubunge ili kupata uwakilishi mpana katika Bunge lijalo na kuwasilisha hoja wanazozihitaji,”amesema Msonga.
“Lakini ninachokiona kama mfuatiliaji wa siasa ni chama kikuu cha upinzani kuwa ajenda ya No reforms, no election, maana yake, hata jitihada za kuwaanda watu kugombea bado hazijapewa kipaumbele, bali kipaumbele kimepewa kutaka mabadiliko yafanyike,”amesema Msonga.
Amefafanua kuwa, haoni jitihada za kuzuia uchaguzi kama zitazaa matunda, ikitokea Chadema ikasusia na vyama vingine vikashiriki, basi uchaguzi huo utakuwa halali.
Ziara ya mafanikio
Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi wa Chadema, Brenda Rupia ameiambia Mwananchi leo Jumatano Aprili 9, 2025 kuwa, ziara yao iliyoanzia wilayani Kilwa Mkoa wa Lindi imekuwa na mafanikio makubwa kuliko changamoto.
“Tumeshahudia mwamko na utayari wa wananchi wa kuibeba ajenda ya No reforms, no election na wameilewa vizuri. Kizuri zaidi kila tunapopita wananchi wenyewe ndio wanaimba No reforms, no election, kumekuwa na mwitikio mkubwa wa wananchi kujitokeza kumsikiliza Lissu,” amesema.
“Changamoto iliyojitokeza ni katika timu ya makamu mwenyekiti (Heche) kuzuiwa mikutano, lakini kila mahali walipozuia kulifanyika utaratibu na mikutano iliendelea kama kawaida. Mwitikio ni mkubwa tofauti na tulivyotarajia, kwa sababu hatukufanya mikutano muda mrefu kanda ya kusini,” amesema Rupia.