
Dar es Salaam. Ahadi nyingine imetolewa kuhusu ujio wa mabasi ya Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT), ikiwa ni ahadi ya tatu kutolewa tangu mwaka huu uanze.
Katika ahadi hii, kwa mujibu wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (Dart), jumla ya mabasi 755 yanatarajiwa kuwasili kati ya Mei na Juni, 2025 na yatatoa huduma katika barabara ya Mbagala.
Mabasi hayo, yatakayotumia gesi asilia iliyobanwa (CNG), ni sehemu ya utekelezaji wa awamu ya pili ya mradi wa BRT na yataletwa na kampuni tatu zilizopewa zabuni ya kutoa huduma katika awamu hiyo, kwa mujibu wa Dart.
Hii ni mara ya tatu kwa ahadi kama hiyo kutolewa kuhusu ujio wa mabasi ya awamu ya pili ya BRT tangu ujenzi wa miundombinu yake ulipokamilika mwaka jana.
Barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 20.3 kutoka Mbagala hadi Gerezani, jijini Dar es Salaam, ilijengwa na Kampuni ya Sinohydro kutoka China na imekabidhiwa kwa Dart.
Ahadi ya awali kuhusu ujio wa mabasi hayo, ilitolewa Januari 2, 2025, na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, aliyesema sekta binafsi italeta mabasi hayo na yangewasili kati ya Februari na Machi, 2025.
Katika ahadi hiyo, alisema mabasi 177 yangetumika kwenye njia ya Kimara, na 755 kwa njia ya Mbagala, na huduma zingezinduliwa Machi.
Ukiachana na Msigwa, ahadi nyingine ilitolewa mwishoni mwa Januari mwaka huu na Mkurugenzi Mtendaji wa Dart, Dk Athuman Kihamia, aliyesema mabasi 250 yanatarajiwa kuwasili kutoka China.
Kwa mujibu wa Dk Kihamia, mabasi hayo yalikuwa katika hatua za mwisho za maandalizi na yangewasili ndani ya miezi miwili hadi mitatu, yaani Machi au Aprili, tayari kuanza kazi.
Alisisitiza kuwa mabasi hayo yatatumia gesi asilia, jambo linalosaidia jitihada za kupunguza uchafuzi wa mazingira nchini.
Katika taarifa yake ya leo, Jumatano, Aprili 9, 2025, Ofisa Habari wa Dart, William Gatambi, amesema mabasi hayo yatawasili kati ya Mei na Julai mwaka huu.
“Kwa kifupi, mabasi yatakuja, lakini sijui chini ya mpango gani hasa yatafika, kwa sababu kuna kampuni tatu tofauti ambazo zitatoa huduma za usafiri wa BRT awamu ya pili. Huenda mabasi yakaanza kuja kwa awamu tofauti tofauti,” amesema.
Hata hivyo, Gatambi hakutaja kampuni zilizopewa zabuni ya kutoa huduma katika awamu hiyo ya mradi wa BRT.
Mbali na suala la mabasi, Dart pia ipo katika harakati za kutafuta wawekezaji kwa ajili ya kujenga miundombinu inayozunguka mfumo wa BRT.
Hii ni pamoja na kupata maeneo ya maegesho kwa bodaboda, magari binafsi, daladala, pamoja na ujenzi wa maduka ya biashara, migahawa na majengo ya kibiashara.
Aidha, Dart inahitaji wawekezaji kwa ajili ya kusimamia matangazo, uuzaji wa majina ya vituo, na shughuli za utangazaji katika baadhi ya vituo vya BRT awamu ya pili, ambavyo ni Mbagala Rangitatu, Zakhem, Maturubai, Kizuiani, Mbagala Sabasaba na vingine.