Ewura kufanya tathmini bei ya umeme

Dar es Salaam. Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), Dk James Mwainyekule amesema katika mwaka wa fedha ujao 2025/2026 wanakusudia kufanya utafiti kuhusiana na gharama halisi za utoaji wa huduma za umeme.

Hili linafanyika baada ya kukamilishwa kwa miradi mikubwa ya umeme iliyofanywa na Serikali, ikiwemo ule wa gesi Kinyerezi na wa uzalishaji umeme wa maji wa Bwawa la Mwalimu Nyerere (JNHPP).

Dk Mwainyekule ametoa kauli hiyo leo Jumatano, Aprili 9, 2025, wakati akitoa salamu zake za utangulizi katika hafla ya uzinduzi wa taarifa ya maendeleo ya sekta ya nishati kwa mwaka 2023/24 unaofanyika jijini Dodoma.

Amesema gharama za utoaji huduma za umeme, ikiwemo bei ya umeme, hazijarekebishwa tangu mwaka 2016, licha ya juhudi za uwekezaji uliofanywa katika miundombinu, na badala yake umefanya hali ya kifedha ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kuendelea kuimarika.

Amesema tathmini hiyo ndiyo itakayoamua iwapo umeme utapanda bei, utashuka au itabakia kama ilivyo, lakini alidokeza kuwa kwa mwaka wa tatu mfululizo Tanesco inatengeneza faida, wakati miaka yote ilikuwa ikitengeneza hasara.

Dk Mwainyekule amesema matumizi ya mitambo ya kukodi katika kuzalisha umeme miaka ya nyuma ilifanya bei za umeme kupanda kwa takribani asilimia 40 mwaka 2011 na asilimia 39 mwaka 2013, lakini hata baada ya kuachana nayo ongezeko la bei za umeme lililowekwa halikushushwa.

Kutoshushwa kwa bei hizo kumeifanya Tanesco kuendelea kuimarika katika upande wa kifedha, na uamuzi wa Serikali wa kubadili deni la Sh2.4 trilioni la Tanesco kuwa lake imeifanya kupata nafasi ya kuboresha mtiririko wake wa kifedha.

“Sasa baada ya kukamilishwa kwa miradi mikubwa ya umeme iliyofanywa na Serikali, ikiwemo ule wa gesi Kinyerezi na ule wa uzalishaji umeme kwa kutumia maji Bwawa la Mwalimu Nyerere katika mwaka wa fedha ujao 2025/2026 tunakusudia kufanya utafiti wa gharama halisi za utoaji wa huduma,” amesema.

Hili linakwenda kufanyika wakati ambao takwimu zinaonyesha kuwa hadi mwaka 2023/2024 kulikuwa na ongezeko la takribani asilimia 26 ya uwezo wa mitambo ya kuzalisha umeme, ambapo megawati 2,411 zilifikiwa, na hadi sasa kama nchi ina uwezo wa kuzalisha megawati 4,032.

Katika kipindi hicho, miundombinu ya kusafirisha umeme iliongezeka kwa asilimia 9, na vituo vya kupoza umeme vilijengwa vinne, na ongezeko la miundombinu ya kusambaza umeme liliongezeka kwa asilimia 15.

“Mwaka 2023 kulikuwa na changamoto ya upatikanaji wa umeme, lakini hadi Februari 2025 tatizo hilo lilifikia ukomo baada ya kuanza kwa uzalishaji umeme katika Bwawa la Mwalimu Julius Nyerere ambapo megawati 490 zilipatikana. Kuongezeka kwa uzalishaji umeme sasa suala la upatikanaji wa huduma limeimarika na sasa changamoto iliyokuwapo zamani imeondolewa,” amesema.

Silvano Msangi, ambaye shughuli yake ni kuchomelea vyuma katika eneo la Kigamboni, amesema anatamani kuona gharama za umeme zikipunguzwa ili kuongeza ufanisi wao katika kazi.

“Natamani tathmini hiyo ije na mapendekezo ya kushushwa kwa bei ili tupate ahueni katika kile ambacho tunakifanya, sasa hivi bei iliyopo inatuumiza sana,” amesema Msangi

Akizungumza kabla ya kuzindua ripoti hiyo, Naibu Waziri Mkuu, Dk Doto Biteko amesema takwimu zinaonyesha kuwa ifikapo mwaka 2035, mahitaji ya umeme nchini yatakuwa megawati 8,055, na mwaka 2030 mahitaji ya umeme yatakuwa megawati 4,878.

Kutokana na kuwapo kwa ongezeko hilo, Dk Biteko alishangazwa na taarifa ya ripoti hiyo inayoonyesha kuwa mikataba 31 ya kuzalisha na kuuziana umeme (PPA) iliyoingiwa nchini haijawahi kuendelezwa tangu kusainiwa kwake. Kati yake, mikataba 21 ni ya uzalishaji umeme kwa kutumia jua.

“Mikataba hii ingetuletea megawati 157, Tanesco fuatilieni mikataba hii ambayo hadi leo haijaanza, mjue kuna tatizo gani na kama kuna sababu ya kuendelea nayo,” amesema Dk Biteko.

“Kuna wakati niliwahi kuwaambia Tanesco wana MOU (mikataba ya makubaliano) mingi – mara ya sola, upepo – ukisaini maana yake umefunga mlango wa mwingine kuingia. Wale mliosaini nao hakuna wanachofanya. Una MOU 57, haipo hata moja. Matokeo yake huwezi kuleta mwingine,” amesema.

Katika kufuatilia mwenendo wa mikataba iliyoingiwa, aliitaka pia Ewura kusaidia ili kujua ni kitu gani wanachoweza kufanya kwa haraka ili wajue nani anafanya na hatua zilizofikiwa,” amesema Dk Biteko.

Hata hivyo, Dk Biteko amesema pamoja na matokeo chanya yaliyoshuhudiwa katika sekta ya nishati, bado inakabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwemo mabadiliko ya tabianchi na uharibifu wa mazingira

Amesema jambo hilo limekuwa kilio kikubwa katika sekta, kwani vyanzo vingine vya maji vinavyotumika kuzalisha umeme vimeharibiwa na kufanya changamoto ya upatikanaji wa umeme kuendelea kuwepo.

“Pia tunakabiliwa na upungufu na uchakavu wa miundombinu, ambao umeendelea kuwa donda ndugu. Hivyo tumeamua kufanya marekebisho makubwa. Maendeleo ya sayansi na teknolojia nayo ni changamoto, kwa sababu kadiri nchi inakua, teknolojia inabadilika na kuleta mahitaji mapya kwenye mnyororo wa nishati,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *